Jaji Mkuu aorodhesha mambo yanayoaibisha mawakili nchini

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 08:54 AM Jul 04 2024
JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma.
Picha: Mtandao
JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amesema ni aibu baadhi ya mawakili kutolipa kodi ya pango ya ofisi zao na wengine kukimbia na fedha za wateja wao baada ya shamba kuuzwa na kupokea malipo hayo.

Amesema mahakama haiwezi kufumbia macho mawakili ambao watakiuka maadili ya kazi zao, akibainisha kuwa wamepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu mienendo ya baadhi ya mawakaili wakati wakifanya majukumu yao ya kazi. 

Prof. Juma alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akiwapokea na kuwakubali mawakili 555, akiwataka wafanye kazi kutokana na kiapo walichokiapa mbele yake kuhusiana na maadili katika taaluma yao. 

Alisema ni jukumu la mahakama kusimamia maadili na kwamba wamekuwa wanapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hivyo Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kijitahidi kusimamia maadili ya mawakili bila kuingiliwa na watu wengine. 

"Ni jukumu la mahakama kusimamia maadili, mfano malalamiko tunayoyapokea mengi mimi, Jaji Kiongozi na wengine ni ya utovu wa maadili, hatuwezi kuyafumbia macho, lazima hatua zichukuliwe," alionya Prof. Juma. 

Jaji Mkuu alisema wananchi (wateja) wanalalamika mawakili kutokurudishia nyaraka halisi pale wanapobadilisha wakili mwingine, akisema jambo hilo ni utovu wa nidhamu kwa kwua ikitokea hali hiyo ni lazima nyaraka hizo zirudi kwa mteja. 

"Changamoto hizi za maadili zinatakiwa zishughulikiwe na TLS wenyewe bila kuingiliwa na ndiyo maana mawakili 100 wa kwanza waliofika mbele yangu niliwauliza 'je! mnafahamu kanuni na kifungu kinachohusiana na maadili?' 

"Ni kifungu kinachoiwezesha TLS katika maadili kwa sababu kila chama kinapaswa kusimama katika maadili. Na kwa bahati nzuri mjiunge katika vyama vya kanda zinazotakiwa kuwasilisha taarifa zinazosimamia maadili," aliagiza. 

Jaji Mkuu pia alisema malalamiko mengine kutoka kwa wanachi ni mikataba wa mauziano ya mashamba; wakili akipata kiasi cha malipo anakimbia na pia wengine hawataki kulipa pango la nyumba (ofisi) zao hadi wamikiliki wamekwenda kulalamika. Ni aibu na ni utovu wa nidhamu. 

"Wengine wanapeleka taarifa mahakamani kuwa wadaiwa wamekubaliana kulipana nje ya mahakama bila wahusika kujua. Wengine wanachukua fedha za wateja hawaonekani mahakamani hadi kesi inafutwa," alisema  

Jaji Mkuu pia aliwataka mawakili hao wasimamie maadili kwa sababu wananchi wanawategemea katika kupeleka malalamiko yao, vinginevyo heshima ya mahakama itashuka.