KLINIKI YA MAKONDA: Tabibu ashauri mwalimu aliyeugua arejeshwe kazini

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 10:12 AM Jul 03 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akimsaidia mgonjwa kupanda kwenye helkopta kupelekewa hospitali ya KCMC.
Picga:Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akimsaidia mgonjwa kupanda kwenye helkopta kupelekewa hospitali ya KCMC.

KAMBI maalum ya madaktari bingwa iliyokuwa inatoa huduma bure mkoani Arusha imebaini mwalimu aliyeacha kazi ya ualimu alikuwa anakabiliwa na tatizo la afya ya akili na uongozi wa mkoa umeombwa kumsaidia arudishwe kazini.

Hayo yalisemwa juzi jioni na Msaikolojia Tiba wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Alex Ndagabwene, wakati akitoa tathmini ya wagonjwa aliohudumia katika kambi hiyo iliyodumu kwa siku nane kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Ndagabwene alisema kuna kesi ya afya ya akili ambayo ilimpata mwalimu ambaye tangu mwaka 2016 alikuwa anapatiwa matibabu bila kutoa taarifa kazini.

"Baadaye anapotea, anakaa nyumbani hadi mwaka ama miwili ndipo anarudi kazini, sasa amejikuta hawezi kupatiwa mshahara wake kwa sababu ameshatolewa kwenye malipo.

"Sisi tumeona changamoto hii kwa sababu alianza kuumwa ugonjwa wa afya ya akili akiwa kazini, alivyorudi nyumbani akawaeleza hawezi kuendelea na kazi kwa kuwa aliona watu wanamtisha kazini na wengine kuwaona ni wabaya ofisini, huu ugonjwa ndivyo unavyoanza," alisema.

Aliongeza kuwa ugonjwa huo una tabia hiyo ya mtu kuacha kazi ndani ya saa 24 au 48 na kuondoka bila kuacha taarifa yoyote kwa kuwa ugonjwa unakuwa umeanza.

Alisema kuwa asipotokea mtu kumfuatilia anaweza asionekane ofisini hadi miaka mitatu ama kuacha chuo bila kutoa taarifa kutokana na shida ya ugonjwa wa afya ya akili.

"Tunaomba uongozi wa mkoa kumsaidia mwalimu huyu arudi kazini kwa kufuata taratibu zinazohitajika, tutashukuru sana," alisema.