Simba yanyakua kocha Morocco

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:54 AM Jul 01 2024
Fadluraghman "Fadlu" Davids.
Picha: Mtandao
Fadluraghman "Fadlu" Davids.

KLABU ya Simba, wakati wowote inaweza kumtangaza raia wa Afrika Kusini, Fadluraghman "Fadlu" Davids kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, atakayekinoa kwa msimu ujao wa mashindano, imefahamika.

Taarifa za ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, baada ya kikao cha juzi mabosi wa Simba kwa kauli moja wamekubaliana kumpa jukumu kocha huyo anayejulikana zaidi kwa jina la Fadlu Davids kuwa Kocha Mkuu ambaye atachukua jukumu la kuongoza kikosi hicho kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA.

"Suala la Kocha Mkuu tumeshamaliza, tunamalizia baadhi ya watu wa benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji wachache waliobaki," alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo.

Fadlu anatua Simba akitoka kocha msaidizi wa kikosi cha Raja Casablanca ya Morocco, ambayo mpaka sasa ipo chini ya Josef Zinnbauer.

Kabla ya kuchukuliwa na klabu hiyo ya Afrika Kaskazini, kocha huyo alikuwa akiifundisha Maritzburg United ya Afrika Kusini, huku 2023 akiwa ni kocha msaidizi katika klabu Lokomotiv Moscow ya Urusi.

Klabu zingine ambazo amewahi kufundisha ni Orlando Pirates ya Afrika Kusini kama kocha mkuu 2021, ambapo kabla ya hapo alikuwa msaidizi kwenye klabu hiyo mwaka 2019, chini ya makocha watatu kwa nyakati toafauti, Zinnbauer ambaye baadaye walikutana Raja Casablanca, Milutin Sredojevic 'Micho', na kocha Rulani Mokwena, kocha wa sasa wa Mamelodi Sundowns.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, alisema suala la kocha linafanyiwa kazi na uongozi wa juu na likikamilika ataambiwa, na yeye atawahabarisha mashabiki.

Pamoja na hayo aliwatoa hofu wanachama na mashabiki wa Simba kuwa watakapoondoka nchini kwenda Misri, kwenye Jiji la Ismailia, watakuwa na benchi zima la ufundi.

"Safari hii niwaambie tu kuwa tutaondoka tukiwa kamili, kwa maana ya makocha wote, mkuu, msaidizi, wa makipa, wa viungo na meneja, kila mtu atakuwa kwenye nafasi yake, pia tutaondoka wote pamoja hapa hapa na wachezaji wote walioongezewa mikataba na wapya, kuelekea kambini kuanza 'pre season' yetu," alisema Ahmed.

Mbali na kocha huyo, Simba ilikuwa inahusishwa na makocha wengine ambao ni Florent Ibenge, ambaye juzi alisema kwa sasa hayupo kwenye mpango huo, Msauzi Steve Khompela  na Mreno Alexandre Miguel Santos ambaye anaifundisha Petro de Luanda ya Angola.

Katika hatua nyingine imefahamika kuwa Simba itacheza mchezo wa kirafiki na APR ya Rwanda wakati wa Tamasha lao la Simba Day litakalofanyika Agosti 3, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Awali Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed wakati akitangaza tarehe rasmi ya tamasha hilo, alisema watatangaza mbeleni timu itakayokuja kucheza na Simba siku ye kilele cha tamasha hilo Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hata hivyo, taarifa kutiko ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Simba imetuma mwaliko kwa klabu hiyo ya Rwanda kuja Tanzania kucheza nao siku hiyo ya kuhitimisha Wiki ya Simba.

Taarifa kutoka Rwanda zimethibitisha klabu hiyo ya jeshi itakuja nchini kucheza na Simba baada ya kukubali mwaliko wa Wekundu hao.

Mtandao maarufu nchini humo (Inyarwanda.com) juzi uliandika, "Agosti 3, 2024, Simba SC watakuwa wenyeji wa APR FC katika mchezo maalum wa Simba Day."

Simba Day ni tamasha la kila mwaka ambalo Simba hulitumia kuwatambulisha wachezaji wake wapya na benchi zima la ufundi mbele ya mashabiki wao.