Simba: Mukwala, Mutale ni ufunguzi, vyuma vinakuja

By Adam Fungamwango ,, Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 11:34 AM Jul 03 2024
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally.
Picha: Mtandao
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally.

BAADA ya jana Simba kuwatangaza rasmi wachezaji wawili, straika Steven Mukwala raia wa Uganda akitokea Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana na winga, Mzambia Joshua Mutale wa Power Dyanamos, imesema kuwa bado inaendelea na usajili mkubwa inaoufanya, ikitamba kuwa kilichoonekana sasa ni sawa na mvua za rasharasha tu, za masika na kwamba kubwa bado.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema hiyo ni asilimia chache tu ya usajili walioufanya, na wachezaji wanaowasajili wote wanaowatangaza wamefanyiwa tathmini kubwa na benchi la ufundi limeridhika na viwango vyao.

"Ni wachezaji ambao ukiwa nao wanakuhakikisha timu yako kupata ushindi, mfano Mutale akiupata mpira pembeni yeye anakimbilia ndani kwenye lango la mpinzani, hakimbii kama msaidizi wa mwamuzi anayekuwa pembeni tu mwa uwanja, si aina ya wale mawinga ambao wanakimbia ili kwenda kupiga krosi, bali yeye mwenyewe anaingia kusababisha hatari, tumepata mtu, ni kijana mdogo ana miaka 22 tu.

"Tayari yupo nchini anasubiri safari ya kwenda Ismailia kuweka kambi ambayo rasmi tumetangaza leo kuwa ni Julai 7, mwaka huu, ndiyo tutaondoka hapa nchini kwenda kuanza maandalizi ya msimu ujao," alisema Ahmed.

Mutale alitambulishwa juzi usiku, huku Mukwala akitambulishwa jana saa saba mchana.

"Mukwala naye ni chaguo sahihi, ana miaka 24 sasa, huyu kijana ndiye alikwenda kumaliza utawala wa kina Emmanuel Okwi na Farouk Miya kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uganda, uzuri na yeye ameonekana kufurahia kuchezea Simba kutokana na rekodi nzuri ya wachezaji wa timu hiyo walioichezea miaka ya nyuma, Okwi na Patrick Ochan," alisema Meneja Habari huyo.

Licha ya timu yake kumaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi ya Ghana, Mukwala amemaliza akiwa nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora nchini humo, akipachika mabao 14, akiongozwa na mshindi wa kiatu cha dhahabu msimu uliomalizika, Stephen Amankona wa Berekum Chelsea FC aliyemaliza na mabao 19.

Straika huyo anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Pa Omari Jobe, ambaye taarifa zinasema atatolewa kwa mkopo kutokana na kushindwa kuonyesha makali yake baada ya kusajiliwa katikati ya msimu uliomalizika.

Kwa upande wa Mutale, anakumbukwa kwa kuwachachafya mabeki wa Simba, hasa Shomari Kapombe, katika mechi ya tamasha la Simba Day Agosti 6, mwaka jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikishinda mabao 2-0, lakini pia aliwafanya anavyotaka katika mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 16, mwaka jana nchini Zambia, timu hizo zikitoka sare ya mabao 2-2.

Mutale alikuwa mwiba kwa mara nyingine katika mechi ya marudiano, Oktoba Mosi, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, zikitoka sare ya bao 1-1, Simba ikitinga hatua ya makundi kwa mabao mengi ya ugenini. Mchezaji huyo amepachika mabao manane kwenye Ligi Kuu ya Soka nchini Zambia msimu uliomalizika.

Baada ya kuachana na nahodha wao, John Bocco ambaye ameondoka na rekodi nzuri za ufungaji kwenye klabu hiyo, na tetesi za kutaka kuachana na Pa Jobe, Mukwala anaonekana kuja kushika usukani kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo akisaidiana na Freddy Michael raia wa Ivory Coast.

“Bado kuna vyuma vingine vipo kwenye mstari wa kutangazwa rasmi, Simba ya msimu ujao inakuja kuwafuta machungu mashabiki wake baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo, tumeleta mashine ya mabao...Mukwala ni zaidi yamshambuliaji na kazi yake itaonekana uwanjani,” alisema Ahmed.