Yanga yamletea mpinzani Aucho

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:28 AM Jul 03 2024
Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.

KLABU ya Yanga iko mbioni kumshusha nchini 'mkata umeme' (kiungo mkabaji) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Onoya Sangana Charve, anayeichezea Klabu ya AS Maniema, ili kuongeza nguvu kwenye eneo hilo ambalo humilikiwa na Khalid Aucho, huku pia ikitangaza rasmi Agosti 4, mwaka huu kuwa ni siku ya Kilele cha Wiki ya Wananchi.

Japo kikosi cha Yanga kina wachezaji wengi mahiri katika eneo hilo ambao ni Aucho aliyeongezewa mkataba wa miaka miwili hivi karibuni, Zawadi Mauya, Jonas Mkude na Mudathir Yahaya, inataka kiungo mwingine ili kusaidiana na waliopo kwa kile kilichoelezwa kuwa na michuano mingi msimu ujao.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo zinasema Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, ameagiza atafutwe kiungo mkabaji mwingine mwenye uwezo kama Aucho kwani akikosekana kutokana na sababu mbalimbali kama vile majeraha, kadi au kufungiwa, pengo lake linaonekana bayana.

"Tumeona ni kweli, misimu miwili eneo hilo linatuponza, tulifungwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na USM Alger ya Algeria kwa sababu tulimkosa Aucho aliyekuwa na kadi, na hatukufanya vizuri dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini hatua ya robo fainali moja kati ya sababu ni kwama hatukuwa na wachezaji wetu nyota wenye uwezo mkubwa akiwamo Aucho kwa sababu mbalimbali, na kuna wakati hapa alikuwa majeruhi, kwa hiyo lazima tupate mtu mwingine," alisema mtoa taarifa wetu.

Alisema, mara nyingi Mudathir anatumika kama mchezaji asiye na namba maalum, anakwenda mbele kusaidia mashambulizi na kurudi nyuma kusaidia kukaba, hivyo tegemeo zaidi kwenye ukabaji ni Aucho pekee.

Mtoa taarifa huyo aliyeongeza kuwa mchezaji huyo amepatikana kwa msaada mkubwa wa Maxi Nzengeli na iwapo mazungumzo yatakwenda vizuri, basi atajiunga na Yanga hivi karibuni.

Akizungumzia kuhusu usajili, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema kwa sasa wanachama na mashabiki watapata pia taarifa za klabu hiyo kupitia simu zao za mkononi ambazo si za kisasa kwa njia ya ujumbe mfupi.

"Mpaka sasa tuna vyanzo mbalimbali vya habari kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambazo zinatoa taarifa, lakini kwa sasa tumeongeza tena huduma nyingine ya kupata habari zetu, inaitwa Yanga Habari, sasa hapo haijalishi shabiki au mwanachana ana simu janja, au zile zinaitwa 'kitochi' zote watatapata taarifa za usajili wa wachezaji na zingine nyingi kwa njia ya ujumbe mfupi," alisema Kamwe.

Akizungumzia siku ya kilele cha Yanga, maarufu kama Siku ya Wananchi, alisema kutakuwa na mkusanyiko wa matukio ya wiki nzima, ikiwamo kuzindua jezi.

"Tarehe nne ndiyo kilele, na watu wanafahamu ni mkusanyiko wa matukio ya wiki nzima, kuna waliokuwa wananiuliza hiyo siku ndiyo tunaanza, halafu tunakwenda kwenye matukio ya kijamii, hapana, hiyo ni siku ya kilele pale Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya hapo siku hizo mbili tatu tutawatangazia siku ya uzinduzi wa jezi na ratiba zingine," alisema Kamwe.