Manji afariki Dunia

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:59 AM Jul 01 2024
Mwenyekiti na mdhamini wa zamani wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti na mdhamini wa zamani wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji.

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mwenyekiti na mdhamini wa zamani wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji amefariki Dunia.

Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa na mtoto wake, Mehboub Manji, ambaye amesema Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya  Quality Group Limited, alifariki dunia  Jumamosi Juni 29, saa 6:00 usiku katika Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa anapatiwa matibabu.

Manji pia aliwahi kuwa, Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mfanyabiashara huyo atakumbukwa zaidi na wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwani aliirudisha kwenye hadhi yake baada ya kukumbwa na migogoro ya mara kwa mara.

Aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake moja ya bahati nasibu, baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.

Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga,  atakumbukwa kwa  kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.

Alipoingia aliikuta klabu ilipodhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.

Moja ya wachezaji ambao waliwasajili kwa kishindo ni kutoka kwa mahasimu wao wa jadi Simba ni Emmanuel Okwi, Kelvin Yondani, Juma Kaseja na ikawapora mchezaji Mbuyu Twite ambaye alikuwa ameshatangazwa na Wekundu wa Msimbazi kutokea, APR ya Rwanda, lakini akaibukia Jangwani.

Baada ya mafanikio makubwa, alijiondoa rasmi kwenye klabu hiyo, 2017, na kuifanya klabu hiyo kuyumba kiuchumi na katika kusaka fedha ilianza kuanzisha Harambee, iliyopachikwa  jina la 'bakuli' hadi pale Kampuni nyingine ya GSM ilipoingia.