Kicheko wakulima wakiuza ufuta zaidi tani 4,000

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:37 AM Jul 01 2024
Zao la ufuta.
Picha: Mtandao
Zao la ufuta.

JUMLA ya tani 4,405 na kilo 472,183 za ufuta zimeuzwa katika Halmashauri za Kilwa, Mtama na Manispaa ya Lindi katika mnada wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao mkoani hapa kupitia mfumo wa Soko la Biashara Tanzania (TMX).

Mnada huo wa pili uliofanyika Kijiji cha Njinjo, Wilaya ya Kilwa umehusisha ufuta wa kwenye maghala ya Nangurukuru Halmashauri ya Kilwa, Bucco, Hazina Manispaa ya Lindi na Ilulu, Halmashauri ya Mtama.

Akitangaza viwango vya bei zilizofikiwa na kampuni zilizojitokeza kununua ufuta huo, Ofisa TEHAMA Goodluck Luhanjo, alisema maghala ya Hazina na Ilulu yaliyopo Halmashauri ya Mtama, yameongoza kwa kuwa na kiwango cha bei za juu.

Akizungumza na wakulima waliojitokeza kwenye mnada huo, alisema ghala la Hazina lilikuwa na tani 510 na kilo 531,021 bei ya juu Sh. 3,482 ya chini Sh.3,450 na Ilulu yenye tani 549 na kilo 854,000 Sh. 3,490 bei ya juu na ya chini Sh.3,400/-.

Ghala la Bucco lililopo Manispaa ya Lindi, tani 1,510 sawa na kilo 1,510,338, bei ya juu Sh. 3,470 na ya chini ni Sh. 3,400, wakati ghala la Nangurukuru lenye tani 1,826 na kilo 1,826,824, bei ya juu imefikia Sh. 3,440 na ya chini ni Sh. 3,340 kwa kila kilo moja.

Mnada umeendeshwa kwa mfumo wa Soko la Biashara Tanzana (TMX), tofauti na ilivyozoeleka kwa wanunuzi kuandika barua wakitaja kiwango wanachokihitaji na bei na kutumbukiza kwenye sanduku, ambalo hufunguliwa na kusomwa na kutajwa bei mbele ya wakulima na wanunuzi wakiwapo siku ya mnada.

Katika mnada huo, kampuni zinazofika bei za juu hupewa fursa kununua mzigo, lakini kwa sasa hufanyika kidijitali kwa njia ya mfumo unaoendeshwa na TMX na kiwango cha tani za ufuta hurushwa mtandaoni, wanunuzi wakishindana kwa kuongeza kiwango cha fedha wanazozinadi na wakulima wakishuhudia kupitia mtandaoni.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakulima Juma Hemedi, Juma Yusufu, Mwanahawa lsmaili, Somowe Abdallah na Hamida Saidi, walisema hawaridhishwi na bei zilizofikiwa na kampuni hizo, lakini wamekubali kuuza kwa shingo upande.

Akizungumzia viwango vilivyofikiwa na wanunuzi Mnumbe alisema zinatokana na mwenendo wa soko, kwa kuwa mazao ya biashara ya ufuta na korosho yanazalishwa nchi mbalimbali duniani, huku akiwasisitiza wakulima kujitahidi mazao wanayozalisha yawe katika ubora unaohitajika.