Msigwa kuhamia CCM wadau wa siasa waibuka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:41 AM Jul 01 2024
news
Picha: Ikulu
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa na Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

BAADHI ya wanasiasa na wachambuzi wa siasa wamesema uamuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatoa tafsiri nyingi ikiwamo nia ya dhati ya kuwa mpinzani nchini.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kiongozi huyo ametumia haki yake kuhama kama ilivyo kwa wachezaji wa mpira, huku wengine wakiona ni anguko la kisiasa hasa kwa wakati alioondoka kwenye chama chake.

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alisema: “Nimeumia sana, alikuwa ‘colleague’ nimekaa naye bungeni, nimekwenda jimboni tumeshirikiana, tamaa yangu kubwa kwamba ningefanya naye kazi CHADEMA kuliko huko alikokwenda, sikutarajia japo nilifahamu alikuwa na hasira kali, nahisi huenda kuna kitu sikufanya kwa rafiki yangu.

“Alikuwa ni ‘partner’ kwenye ‘struggle’ sioni sawa kwa Msigwa kwenda kufanya kazi na CCM, katika siku za mwisho za kuiondoa CCM madarakani,” alisema.

“Huenda alikuwa na hasira kali sana ambayo huenda sikuielewa, ningejua ningetumia muda wangu kama rafiki kumshauri huenda asingeenda,” alisema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisema chama kilikuwa na taarifa za kiintelejensia kwamba hana muda mrefu ataondoka, na kwamba vurugu zote alizokuwa anafanya kule Kanda ya Nyasa ilikuwa ni maandalizi kuelekea CCM.

“Chama tulishaona, tunatarajia atazungumza mambo mengi ya kweli na yasiyo ya kweli atayaacha, tunawataka wanachama wetu kule Nyasa kuendelea na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Yeye sio wa kwanza kuhama walikuwapo wengi maarufu kuliko yeye waliondoka na chama hakikuwahi kuyumba na tunaendelea kujenga chama.”

Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Morogoro, Devotha Minja alisema: “Ninachokiona kuwa mpinzani kwa miaka mingi halafu unatimka kisa umekosa nafasi ya kanda sio sawa, maana yake tulikuwa na mtu ambaye sio mpambanaji, hakuwa na nia ya dhati, kwasababu alichokuwa anakipinga ni serikali leo ameamua kuungana nayo, maana yake hakuwa mpigania haki kwa Watanzania.

Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob alisema: “Sidhani kama ni uamuzi sahihi kwa namna yoyote, kwanza kahama kipindi kibaya kwa sababu kashindwa uchaguzi, kila mtu anajua kwamba kashindwa uchaguzi.

“Mtu akihama kwa sasa sio msimu mzuri ni kama amesubiri jua au mvua inyeshe ndio atoke, kipindi cha nyuma walikuwa wanapewa ofa mbalimbali. Mwenendo wake ulionyesha alishakata tamaa,”alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa, alisema mwanasiasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine ni jambo la kawaida, na kwamba ni haki yake mtu yeyote kwenye chama.

Alisema anachokiona ndani ya chama hicho ni matokeo ya kutoelewana kwao katika chaguzi za ndani ya chama, na wasingeweza kuendelea kukaa pamoja labda kama pangefanyika jitihada za kumaliza mgogoro.

“Moja ya matatizo tuliyonayo ndani ya vyama hakuna mfumo wa kumaliza tofauti na watu waende vizuri, kwenye chama chochote unapogombea nafasi atatokea mmoja ashinde na mwingine anakosa, kama chama kingekuwa na utaratibu wa kuwaweka mambo sawa maana yake wangeyazungumza ndani kwa ndani,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Kahangwa, Msigwa hawi mwanasiasa wa kwanza kwa kuwa wapo wengi walitoka wakaenda CCM au CHADEMA, na kwamba siku zote wanasiasa ni watu wa kuvizia fursa, hivyo ameona katika uchaguzi mkuu kuna mambo yanaweza kwenda vizuri kwake.

“Siasa ni kama mpira leo ni mchezaji wa timu fulani kesho ni nyingine. Lakini wanasiasa wetu pamoja na haki yao ya kuhama wakumbuke kuwa wakweli, ukisikiliza ‘speech’ (hotuba) zake ikiwamo neno maarufu la ‘You guys are tired’ ambalo alilitumia sana akiwa bungeni, usingefikiri kwa kauli hizi angekuwa ni mtu angefika mahali akaondoka, ingawa ni haki yake,” alifafanua.

Alisema wanasiasa wanapaswa kuwa na busara ya kuwa mtu kutamka masuala yanayohusu maslahi ya watu bila kuponda wengine ambao kesho atajiunga nao na ni hekima inayopaswa iwaongoze wanasiasa wetu, kwa kuwa ukiitukana CCM halafu kesho ukahamia huko unakuwa umepoteza kuaminika. 

Mchambuzi wa siasa na Mwanadiplomasia, Hamduni Maliseli alisema: “Inaonyesha dhahiri watu tulionao (wanasiasa) ni watu wa aina gani dhidi ya upinzani, wamekaa kwenye upinzani kwa ncha za vidole na sio mguu kamili, kwa sababu hakupata fursa ya kuwa katika uongozi basi kaenda CCM.”

“Hii inaonyesha upinzani wa baadhi ya watu hauna uhalisia ni matokeo ya kusaka tonge akikosa kulia apate kushoto. Msigwa amekuwa kiongozi aliyeaminika sana kwenye jamii, kitendo cha kuhama kwasababu ya kukosa uongozi, inaonyesha tu safari, bado kuna mzaha na hakuna watu wanaoamini katika itikadi na falsafa ya chama fulani kwa dhati ya moyo ndio mana wanachomoka hovyo,” alibainisha.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, Msigwa kwenda ni haki yake, lakini tatizo ni mtu wa aina gani, ana nafasi gani, alizungumza mangapi kuhusu uimara na uthabiti wa upinzani, nguvu yake na kwamba asipoangalia inaweza kuwa ndio mwisho wake.

“Taswira sio upinzani bali hata nafsi inaweza kumsuta hata yeye mwenyewe,” alisema.

Mwandishi wa habari nguli, Absalom Kibanda alisema: “Nimejifunza kwamba usiwapime wanasiasa kwa maneno yao bali kwa kauli zao, kauli zake zilionyesha ndiye anakerwa sana na watu wanaohama kwenda CCM, alimkosoa sana Mwenyekiti wake Freeman Mbowe alivyokwenda kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan, na kila mahali alisema angehama enzi za Rais Dk. John Magufuli, alionyesha ni mwanaCHADEMA kindakindaki.”

“Ila inanikumbusha kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwamba CCM sio baba yangu wala mama yangu,” alisema.

Kibanda alisema Msigwa alikuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa aligombea na kushindwa maana yake angeshinda angeendelea kubaki na alikata rufani kudai haki yake leo anahamia CCM inaibua maswali mengi kuhusu siasa na wanasiasa wa vyama vingi.

Msigwa ambaye ni Mbunge mstaafu wa Jimbo la Iringa Mjini, alitangaza uamuzi wa kukihama CHADEMA, alipokewa jana wakati wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan.