Tisa wapandishwa kizimbani kwa shtaka kumuua Asimwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:24 AM Jun 29 2024
Tisa wapandishwa kizimbani  kwa shtaka kumuua Asimwe.
Picha: Mtandao
Tisa wapandishwa kizimbani kwa shtaka kumuua Asimwe.

WATU tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kagera kwa tuhuma za mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2).

Asimwe aliuawa na kukatwa viungo vyake vya mwili na kisha mwili wake kutelekezwa katika kalavati wilayani Muleba, mkoani Kagera.

Washtakiwa hao walifikishwa jana mahakamani huko ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu kuripotiwa tukio hilo Mei 30 mwaka huu katika Kata ya Kamachumu, wilayani Muleba.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Elipidius Rwegoshora na Novart Venant, ambaye ni baba mzazi wa mtoto Asimwe.

Wengine ni Ramadhani Selestine, Nurdin Masoud, Rwenyagira Burukadi, Dunstan Burchard, Faswiu Athman, Gozbert Alchard na Dezdery Evergist ambao walisomewa shtaka moja la mauaji ya kukusudia.

Walisomewa shtaka hilo na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kagera, Waziri Magumbo, aliyesaidiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Erick Mabagala, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Elipokea Yona Wilson.

Magumbo alidai kuwa uchunguzi wa shauri hilo namba 17740 la mwaka 2024 umekamilika. Hakimu Wilson aliahirisha shauri hilo hadi Julai 12 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa walirejeshwa rumande kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Mei 30 mwaka huu, mtoto Asimwe aliripotiwa kuporwa kwa mama yake mzazi na watu wasiojulikana waliodaiwa kutokomea naye.

Juni 17 mwaka huu, mwili wa mtoto huyo ulikuwa katika kalavati, huku Jeshi la Polisi likieleza kuwa baadhi ya viungo vyake vilikuwa vimenyofolewa.