Ubunifu, uwekezaji kwenye zana za kisasa matrekta yanayolima, kupanda, kusindika…..

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:41 PM Jul 01 2024
Mkulima wa  minazi Gideon Mwendiumi, anayemiliki zaidi ya ekari 11 za zao hilo wilayani Mkuranga,  akitoa maelezo ya namna bora ya kulima nazi kwa  tija.
PICHA: MAULID MMBAGA .
Mkulima wa minazi Gideon Mwendiumi, anayemiliki zaidi ya ekari 11 za zao hilo wilayani Mkuranga, akitoa maelezo ya namna bora ya kulima nazi kwa tija.

UWEKEZAJI kwenye zana za kisasa kuanzia matrekta, mbegu bora na miundombinu ya kilimo isiyotegemea mvua wala kuathiriwa na ukame ndiyo njia ya kuwaondoa vijana kwenye chuki dhidi ya kilimo.

Ni maoni ya wadau wa kilimo, wanaoeleza kuwa mapinduzi ya kilimo hayatokani na kingine bali zana bora, mbegu na matumizi ya teknolojia shambani ili kuongeza mnyororo.

Wanataja zana hizo kuwa ni pamoja na matrekta makubwa kwa madogo ya kulima, kupanda, kupalilia, kunyunyiza dawa, kuvuna na  kuchakata zikipatikana zitawavuta vijana kupenda kilimo lakini, pia kukuza uchumi, kumaliza njaa  na  kukabiliana na uhaba wa ajira.

Akizungumza na Nipashe kwenye shamba darasa linaloandaliwa na Kituo ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Mikocheni Dar es Salaam,  mkulima Gideon Mwendiumi, anasema zana za kisasa na teknolojia ni muhimu katika kurahisisha uzalishaji shambani.

Anasema Marekani, China, Russia, Ufaransa pamoja na Misri kwa upande wa Afrika zimepiga hatua kubwa katika sekta ya kilimo kutokana na kutumia vifaa vya kisasa kuzalisha mazao mbalimbali pamoja na mamilioni ya tani za vyakula kwa mwaka.

Mwendiumi meneja mstaafu wa kituo cha TARI, anaeleza kuwa ili kilimo kibaki uti wa mgongo na kutoa ajira kwa vijana, lazima serikali iweke mkakati wa kuwekeza vifaa vya kisasa na kuwapatia wakulima ili kuongeza kasi na tija ya uzalishaji, akisema  vijana wengi wanakikimbia kutokana na ugumu wa kukiendesha.

“Wakulima wengi wanaona kama kilimo ni utumwa kwa sababu ya kutumia jembe la mkono.  Mataifa makubwa yanatumia matrekta madogo kwa makubwa kulima maeneo makubwa kwa muda mfupi, kadhalika kuyahudumia na kupata tija kwa wepesi na kwa ufanisi.

 “Tukiwekeza katika zana za kisasa vijana hawatakata tamaa, kumekuwa na malalamiko kwamba wengi wanakimbilia mjini, ni kwa sababu wameona wazee wanapinda mgongo ni shida ya kushika jembe, wakaona hii kazi hatuiwezi twende mijini. Wapo wanafanya kazi za ovyo, nia yao wapate fedha, hivyo tukiboresha wengi watalima,” anashauri Mwendiumi.

ALILIA MINAZI

Mwendiumi, mkulima wa nazi wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani, anasema kilimo hicho kinawasaidia wengi kwasababu upatikanaji wa nazi nchini ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji, akieleza kuwa matumizi ya bidhaa hiyo pamoja na mafuta yake bado ni makubwa licha ya kilimo chake kuwa chini.

“Kilimo cha minazi kinashuka kwa sababu nyingi, mfano Mkuranga  wilaya inayoongoza kwa viwanda vingi, ujenzi wake umesababisha minazi mingi kukatwa na hakuna  juhudi za kuipanda.

“Hali hiyo inasababisha upungufu wa nazi kwenye soko kuwa mkubwa, nimeona huko mtaani wengi wameanza kuhamasika kutaka kupanda minazi baada ya kuona moja inafika mpaka 1,000. Wanasema kumbe inaweza ikawa sehemu ya ukombozi.

“Lakini kilimo cha mnazi ni kigumu, ugumu wake uko kwenye mambo matatu magonjwa, wadudu na maandalizi ya kuhakikisha zao linakuwa katika maeneo yanayouzika, kwa sababu elimu ya upandaji ni ile iliyozoeleka na mababu zetu toka miaka hiyo.”

Anataka elimu itolewe sambamba na kuwekeza katika teknolojia ili watu walime kwa urahisi huku wakiwa na uelewa, ndiyo maana kituo cha TARI Mikocheni kinahamasisha watu kujua umuhumu wa kuchagua mbegu bora wakishirikiana na wataalamu ili kupunguza athari za magonjwa.

MKAKATI  KUINUSURU

Meneja wa kituo cha TARI Mikocheni Dk. Fred Tairo, anasema kuna mkakati wa kufufua kilimo cha nazi  kwa kuendesha utafiti, kutenga ardhi na fedha kwa ajili ya kupatia vikundi vya vijana watakaokuwa na utayari wa kujihusisha na kilimo cha zao hilo.

Dk Tairo anaeleza kuwa baada ya vijana kupata mafunzo watapatiwa eneo, mbegu na fedha kwa ajili ya huduma za kilimo mpaka watakapofikia hatua za kuvuna mbegu na kuziuza, na kwamba fedha itakayopatikana watarudisha kiasi na nyingine wataitumia kujiendeleza.

“Kwa muda mrefu nazi imesahaulika kwa sababu mbalimbali na kusababisha kushuka uzalishaji lakini serikali imeamua kulifufua kwa ajili ya kuongeza tija, ikiwemo pia kufufua mashamba mapya na kuendeleza ya zamani na kusambaza kwa wakulima takribani  mbegu milioni 10 kwa mwaka.

“Changamoto inayowasibu vijana wengi hawana taarifa ya hizi za fursa ambazo zipo, ndiyo maana serikali imeamua kutenga fedha kwa ajili ya kuwashawishi vijana waingie kwenye hizo fursa kama njia ya ajira, mojawapo kuanzisha vitalu na kukamua mafuta, sisi tunavyowasiliana nao tunawapa elimu pana kwa mnyororo wa thamani wa zao la Nazi,” anasema Dk. Tairo.

Vile vile, anaeleza kuwa wamekuwa na program ya kuwasaidia wakulima katika masuala mbalimbali ya kitaalamu, pamoja na kuongeza tija, huku akiwashauri kuachana na utaratibu wa kuuziana nazi shambani badala yake wawe na utaratibu maalum ili kuongeza thamani.

"Nasisitiza katika suala la kuongeza thamani ya bidhaa hii kwasababu nazi ile ya kula nyumbani ambayo ataiuza kwa Sh 800 hadi 1,000 ndiyo inayotumika kutengeneza mafuta ambayo sokoni gharama yake itamnufaisha zaidi mkulima na kituoni kwetu tumeboresha mashine za kukamua na kuchuja mafuta.

Ofisa Kilimo Msaidizi Mkuu TARI Mikocheni, Violeth Kiwia, anasema nazi ni muhimu kwasababu zinahitajika katika chakula na kutengeneza thamani mbalimbali ambazo zina soko kubwa linalotoa fursa za ajira ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Ally, anasisitiza maofisa ugani kutoa majawabu ya changamoto zinazowakabili wakulima wakiwamo wanaojihusisha na nazi, na kuwafanya waone umuhimu wa kuweko kwa wataalamu hao katika kufanya kilimo endelevu na chenye tija katika maeneo yao.