Wanafunzi 700 wanufaika na taulo za kike Shule ya Sekondari Mzimuni

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:23 PM Jul 03 2024
Wanafunzi 700 wanufaika na taulo za kike Shule ya Sekondari Mzimuni.
Picha: Maulid Mmbaga
Wanafunzi 700 wanufaika na taulo za kike Shule ya Sekondari Mzimuni.

WANAFUNZI 750 katika Shule ya Sekondari Mzimuni iliyoko Halmashauri ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam wamekuwa na uhakika wa kuendelea na masomo bila kukutana na changamoto ya hedhi, baada ya kupatiwa msaada wa taulo za kike na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundatio (AMF).

Akizungumza leo baada ya kutoa msaada huo Mkurugenzi wa taasisi hiyo Asma Mwinyi, amesema lengo kubwa la kutoa taulo hizo ni ili kuwasaidia wanafunzi wa kike wasikose masomo kwa kutoingia darasani kwasababu ya hedhi.

Amesema jitihada hizo pia ni ili kwenda sambamba na kuiishi kaulimbiu yao ya (Nisitiri Nisifedheheke) na kwamba mkakati wao ni kuwafikia wanafunzi 30,000 kwa Tanzania Bara na visiwani, ambako hadi sasa wasichana zaidi ya 20,000 wameshapatiwa.

"Kila mwanafunzi atapata pakiti sita na kila moja ina taulo 10 ndani, tunaimani zitaenda kuwasaidia watoto wetu kwa kiasi kikubwa, tutaendelea na kampeni hii katika kuwasaidia wenye uhitaji Tanzania nzima," amesema Asma.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (UWT) Mkoa wa Dar es Salaam, Khadija Ally, amesema hedhi imekuwa ni tatizo kwa wanafunzi wa kike nchini, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na AMF katika kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji wasifedheheke.

Pia ametoa wito kwa walimu wa shule zote nchini wakisaidiana na wazazi kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao na kamwe suala la hedhi lisije likawa chanzo cha kuwafanya washindwe kufikia matarajio yao.

"Niwaombe watoto wakike munapofikia hatua ya mabadiliko ya kimwili mukajitunze, musikubali kufedheheka, mukawe mfano katika kusimamia malengo yenu, tunatarajia baadae mje kuwa viongozi na mkawe msaada kwa wengine," amesema Khadija.

Akizungumzia wanafunzi wa kiume, alisisitiza kuwa mwalimu bora ni yule aliyekuwa rafiki kwa wanafunzi wote na kujua matatizo yanayomkabili na kumsaidia kuyapatia ufumbuzi, akieleza kuwa takwimu za masuala ya ulawiti kwa watoto hadhiridhishi na zinatisha, hivyo wasaidiane katika malezi kuwalinda watoto hao.

"Vijana wetu taifa liko mikononi mwenu mkae na imani mkazingatie tamaduni za kitanzania, unapofanyiwa chochote msikae kimya semeni, na msikubali kuharibiwa ndoto zenu, kasimamieni malengo yenu," alisisitiza Khadija.

Mkuu wa shule hiyo Juma Lighton, alisema katika kuhakikisha wanafunzi wakike wanasaidiwa na hawakosi masomo wakati wa hedhi, katika shule hiyo wametenga bajeti ya kununua taulo pamoja na kuweka chumba maalumu kwaajili ya wanafunzi kukitumia kujisitiri wakiwa katika hali hiyo.

Rahma Shabani, mmoja wa wanafunzi waliopatiwa msaada huo, alisema taulo hizo zitawasaidia kujiamini wakiwa darasani hasa wakati wa kipindi cha hedhi.