Hai yapangua hoja ya CAG, vituo 30 vya afya

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 05:51 PM Jul 03 2024
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akitoa maelekezo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Hai, kuhusu hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Picha: Godfrey Mushi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akitoa maelekezo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Hai, kuhusu hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

HATIMAYE Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, imepata ‘mwarobaini’ wa kudumu wa hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya kupoteza mapato kutokana na kutosimikwa kwa Mfumo wa Ukusanyaji Mapato wa Kielektoniki (GoT-HOMIS) katika Vituo 30 vya Afya vya Halmashauri hiyo.

Tayari, Halmashauri hiyo imetenga Sh. milioni 18.1 katika bajeti ya mwaka ya mwaka wa fedha 2024/2025, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ufungaji wa mfumo huo mpya, ambao unatarajiwa kufungwa mwezi Julai mwaka huu katika vituo vyote vya afya.

Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo, Oscar Sabachua, wakati anawasilisha Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani, lililoketi jana kujadili hoja hizo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka 2023, amesema utekelezaji huo ni mahitaji ya agizo namba 31 la mawanda ya fedha ya mwaka 2009.

Kwa mujibu wa Sabachua, hivi sasa vituo vya kutolea huduma za afya vinane, vimesimika Mfumo huo wa GoT-HOMIS. Vituo hivyo ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Hai, Kituo cha Afya Kisiki, Kituo cha Afya Nkwansira, Kituo cha Afya Masama-Mbweera, Kituo cha Afya Lyamungo, Kituo cha Afya KIA na Kituo cha Afya Mashua.

“Hoja ya Kutosimikwa kwa Mfumo wa Ukusanyaji Mapato wa Kielektoniki (GoT-HOMIS) katika Vituo 30 vya Afya vya Halmashauri. Mapendekezo ya CAG yalikuwa ni, Halmashauri itenge bajeti kwa ajili ya kufunga mfumo wa mapato ya kielektroniki na vifaa vyake vinavyosaidia kuhakikisha kwamba mfumo huo unatumika, na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

“Majibu ya Menejimenti. Menejimenti imeendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinafungwa mfumo huo ili kuboresha ukusanyaji wa mapato.”amesema Sabachua, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dionis Myinga.

Mfumo wa Government of Tanzania – Health Operationts Management Information System (GoT-HOMIS), ambao ni wa kielektroniki, umewekwa kwa lengo la usimamizi wa shughuli za uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini.

Kufungwa kwa mfumo huo, na kuanza kutumika utasaidia kurahisisha shughuli za vituo vya kutolea huduma za afya na kusimamia uzalishaji na uhifadhi sahihi wa taarifa na takwimu za wagonjwa na magonjwa, mapato na dawa za vituo vya kutolea huduma za afya.

Mfumo wa GoT-HOMIS, utasaidia vilevile katika kuboresha huduma za afya nchini na kuleta tija ya upatikanaji wa haraka wa takwimu mbalimbali na kwa wakati, na kusaidia kujua matumizi ya dawa hadi ngazi ya mtoa huduma.

Aidha, Mfumo huo wa GoT-HOMIS, utachochea ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya kituo, kwani mfumo huu utaonyesha mapato sahihi ambayo yanakusanywa na kituo husika.