Rais Samia asisitiza ushirikiano kati ya serikali na taasisi za dini

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 06:15 PM Jul 03 2024

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea picha kutoka kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Wolfgang Pisa.
Picha: Mary Geofrey
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea picha kutoka kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Wolfgang Pisa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ufanyaji kazi kwa ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi za Dini nchini ili kuendelea kujenga amani, umoja na mshikamano.

Amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi hizo ambao huleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa.

“Tunashukuru tunapata ushauri, yapo mambo ambayo mnayafanya na kuiwezesha nchi hii iendelee, mshikamano wetu ndani ya nchi, umoja wetu ndio unaozaa utulivu na amani tuliyonayo,” amesisitiza.

Amesema hayo wakati akiwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais  Samia leo Jumatano, Julai 03, 2024 kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Wolfgang Pisa.

Askofu Pisa pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, kwenye makazi ya maaskofu, Mtanda mkoani Lindi.

Amesema kuwa, serikali itaendelea kumpa ushirikiano wa dhati. “Wakati wote utakapokuwa na jambo ambalo unadhani serikali inahitaji kushauriwa uwe huru na wakati wote unapoona kwamba unahitaji kuunganisha nguvu na serikali, sisi tutakupa ushirikiano,” amesema.

Ameongeza kuwa serikali kwa upande wake imeshaagiza ushirikiano huo usiwe tu ngazi ya kitaifa bali uende hadi katika ngazi ya vitongoji.

“Tuendelee kuwa pamoja na kuja kwangu hapa nikuhakikishie tunaendelea kukupa ushirikiano,” amesesisitiza.