Viwanda 25 kutoka China vyashiriki maonyesho Sabasaba

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:06 PM Jul 01 2024
Baadhi ya watembeleaji wa maonyesho ya Sabasaba wakiangalia bidhaa kwenye banda ya Wachina.
Picha: Elizabeth Zaya
Baadhi ya watembeleaji wa maonyesho ya Sabasaba wakiangalia bidhaa kwenye banda ya Wachina.

VIWANDA 25 kutoka nchini China vinashiriki maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba chini ya uratibu wa Kampuni za Usafirishaji Mizigo za Kitanzania za DM Mall na MMG Logistics.

Mkurugenzi  wa kampuni hizo Hamid Idrissa amesema lengo la ujio wa kampuni hizo ni kuonyesha bidhaa wanazozalisha, kutengeneza mtandao na wafanyabiashara wa Tanzania pamoja kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwavuta wawekezaji kutembelea nchini na kuona fursa zilizopo.

Ametaja miongoni mwa viwanda vilivyokuja ni pamoja na vya nguo, vifaa vya majumbani, simu, solar, viatu, mitambo, vinywaji, Jenereta, magari, vyakula, bidhaa za urembo na bidhaa mbalimbali ambapo pia, watatumia maonesho hayo kuuza na kuonesha shughuli zao.

"Lengo la kuwaleta hatutaki kikundi cha watu kinufaike peke yao bali Mtanzania mmoja mmoja anufaike na apate bidhaa kwa bei ndogo ili kuyavutia makampuni hayo kuwekeza nchini na hatimaye kufungua viwanda na  kutoa ajira nyingi  kwa vijana," amesema Idrissa.

Meneja Masoko wa DM Mall na MMG Logistics, Haruna Said alisema baada ya kuona changamoto wanazopitia Wafanyabiashara wa Kitanzania, vijana wa Kitanzania waliosoma China waliona kuna haja ya kuwasaidia wafanyabiashara kwa kuwaunganisha na makampuni ya China kufanya biashara na kupata mizigo yao kwa wakati.

Amesema tangu wameanza ushirikiano na makampuni mbalimbali ya Kichina  kwa ajili ya kufanya biashara na wafanyabiashara wa Tanzania kwa zaidi ya  miaka mitano, wameajiri vijana zaidi ya 35 hapa nchini na China pamoja na Wachina wanane.

"Natoa wito kwa Watanzania waone fursa kupitia makampuni haya, tuna ushirikiano mzuri, bidhaa zao ni bei poa wakija na kutaka kufanya kazi na sisi watanufaika na nchi itaendelea kupata mapato kwa ajili ya kufanya maendeleo ya nchi, waje hapa Sabasaba kwenye Banda la Kichina waone bei za bidhaa kuanzia Sh.100 kwa bei ya promosheni,"amesema.

Amesema ujio wa wafanyabiashara hao ni kutaka kuonyesha umakini kwa kutangaza bidhaa zao halisi zenye ubora zikitoka katika miji tofauti ya China.

Ametoa wito kwa wafanya biashara wanaotaka kusafirishiwa bidhaa zao kupitia kampuni hiyo ili kuwasaidia kufikisha kwa wakati.

"Imezoeleka mtu anapoagiza mzigo wake kutoka china hufika Tanzania kwa kuchelewa lakini kampuni zetu ni za uhakika katika kufikisha bizaa kwa wakati kufuatana na matukio kama siku za sikukuu.

"Sabasaba tutakuwa na zawadi tofauti tofauti kwa bei za kawaida ikiwa ni sehemu ya kutangaza bidhaa zetu lengo ni kutaka watu wapate vitu bora.

Miongoni mwa wafanyabiashara kutoka Kampuni ya  XY Cargo Feler Logistics ya China Xu Jian, amesema wamechagua kuja Tanzania kwa kuwa ni sehemu salama kwa kufanya biashara lakini pia, wakitegemea  kupata wateja wengi wa kushirikiana nao.

Wawakilishi wa viwanda hivyo wanatarajia kukutana hivi karibuni na wafanyabiashara wa Tanzania kubadilishana ujuzi ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Mipango na uwekezaji Professa Kitila Mkumbo.