Mstaafu Kikwete atoboa siri ya ushindi wa CCM

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:22 PM Jul 01 2024
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete  amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi leo tarehe 01, Julai, 2024 katika ofisi yake binafsi Masaki jijini Dar es Salaam.
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi leo tarehe 01, Julai, 2024 katika ofisi yake binafsi Masaki jijini Dar es Salaam.

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema anafurahishwa na namna makada, wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, wanavyoendeleza umoja miongoni mwao.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, amesema umoja miongoni mwa wanachama ndio nguzo na silaha muhimu hasa wakati huu wa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Kikwete ameyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi aliyemtembelea kumjulia hali kwenye ofisi yake binafsi, jijini Dar es Salaam.

Rais Mstaafu Kikwete ametumia nafasi hiyo kumwambia Nchimbi kwa jinsi anavyofurahishwa na namna maelekezo anayotoa Mwenyekiti wa CCM Dk. Samia ya kuwataka viongozi wa Chama kushuka chini kwa wanachama na wananchi kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao, yanavyotekelezwa kikamilifu.
Aidha, ameipongeza sekreterieti mpya ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa jinsi inavyojikita katika kuimarisha chama na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya 2020 -2025 kwa wananchi.

“Umoja na mshikamano wa wana-CCM ndiyo umekuwa siri na silaha ya ushindi, ndiyo maana tunasema siku zote umoja wetu ndiyo ushindi wetu. Tunafurahia sana tunavyoona wana-CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti Dk Samia Suluhu Hassan wanaendeleza kuimarisha msingi huo. Hongereni sana," amesema Kikwete.

Kwa upande wake, Balozi Nchimbi amewashukuru viongozi wastaafu wa Chama na Serikali kwa jinsi wanavyofanya kazi ya kuwalea kiuongozi na kimaadili viongozi wa sasa.

Amesema CCM itaendeleza utamaduni wa kuwaenzi na kuwasikiliza viongozi wastaafu.Nchimbi amesema kwa uzoefu wa uongozi na kazi nzuri ya kulitumikia taifa waliyofanya wakati wa uongozi wao, viongozi hao ni hazina kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.