NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, ameshangazwa na idadi ndogo ya waombaji wa nafasi za kazi kada ya afya waliokuwa wameomba katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Lindi na Mtwara.
Wakati waombaji katika mikoa hiyo ikiwa ndogo, mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma ina idadi kubwa ya waombaji kulinganisha na uhitaji.
Hatua hiyo imetokana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuweka utaratibu wa kuomba ajira katika mkoa husika kulingana na uhitaji.
Juni, mwaka huu, sekretarieti hiyo ilitangaza nafasi za kazi 9,483 za kada ya afya na kila mwombaji alitakiwa kuomba ajira katika mkoa ambao atafanya kazi endapo atafanikiwa kupita kwenye usaili.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, licha ya tatizo kubwa la ajira linalowakumba vijana wengi, bado waombaji wanataka kuanza kufanya kazi katika majiji makubwa jambo ambalo ni gumu.
Sangu alisema hayo juzi alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, ikiwa ni mwendelezo wa kliniki ya kimkakati ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao.
Alisema mkoa wa Kigoma, kwa mfano, mahitaji halisi ya waliotakiwa kuajiriwa katika kada ya afya yalikuwa watumishi 400 lakini waombaji wa nafasi hizo walikuwa hawazidi 200 huku mikoa ya Lindi, Mtwara na Katavi nako idadi ikiwa ndogo kulinganisha na uhitaji.
Kutokana na hali hiyo, Sangu alitoa wito kwa wazazi kuwashawishi watoto kuomba ajira pindi zinapotangazwa katika mikoa hiyo kwa kuwa uwezekano wa kupata ni mkubwa kulinganisha na mikoa kama Arusha na Dodoma ambako ushindani ni mkubwa.
Aidha, Sangu aliwaonya wale watakaoomba kazi katika mikoa hiyo halafu wakapangiwa wanaanza kuomba uhamisho. Alisema serikali haitawavumilia endapo wataanza kufanya hivyo kabla ya kufanya kazi kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
Naibu Waziri alisisitiza kuwa mikoa hiyo haina tofauti na Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na Arusha kwa kuwa ina fursa za kiuchumi na miundombinu iliyoboreshwa. Aliwataka uhitaji wa ajira kuchangamkia zinapotangazwa kwenye mikoa hiyo.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abert Msovela, alisema licha ya uwapo wa fursa za kiuchumi katika mkoa huo, bado idadi ya watumishi wa umma wanaotuma maombi ya kutaka kuhama ni kubwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED