HATIMAYE kikosi cha JKT Tanzania kinatarajia kurejea dimbani baada ya siku 29 kucheza dhidi ya Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa timu hiyo, tangu Oktoba 26, mwaka huu, ilipocheza mechi ya mwisho dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Jamhuri Dodoma, kabla ya kupata ajali Oktoba 30, mwaka huu jijini, Dar es Salaam na kusababisha majeruhi kwa wachezaji wao 11.
Baada ya hapo, Bodi ya Ligi iliahirisha baadhi ya michezo ya timu hiyo ili kuwapa muda wachezaji kuimarika afya zao.
Mechi zilizoahirishwa ni dhidi ya Simba na Namungo, lakini leo inarejea uwanjani, huku Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire, akisema wachezaji wao wote wameshapona, wamefanya mazoezi na wapo fiti kwa mchezo huo.
"Tumejiandaa na mchezo huu, tunajua muda mrefu hatujacheza ligi, hivyo tunahitaji pointi tatu ili tujiweke vizuri katika msimamo, alisema Bwire.
JKT Tanzania ambayo imecheza michezo tisa tu, inashika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 10 sawa na wapinzani wao, Prisons ambao wanafuatiwa katika msimamo huo lakini wameshacheza michezo 10.
Kuelekea kwenye mchezo wa leo, Kocha Mkuu wa Prisons, Mbwana Makata, aliwapeleka wachezaji wake 'gym' kwa ajili ya kuwaongezea utimamu wa mwili kwa sababu wanakwenda kucheza na timu ya maafande kama wao.
"Lazima tuongeze dozi, wachezaji wakiwa na fiziki sawa sawa watakuwa na pumzi, spidi na kufanya kila unachowaelekeza, hasa tunapokwenda kucheza na JKT Tanzania ambayo pia ni timu ya maafande kama sisi," alisema kocha huyo.
Mbali na mechi hiyo, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi leo Tabora United itawaalika Singida Black Stars huku Dodoma Jiji ikiwa mwenyeji wa KMC kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED