MAMIA ya Watanzania wakiongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Damas Ndumbaro, Jumatatu iliyopita walimiminika kwenye viwanja wa Leaders, jijini Dar es Salaam, kumuaga mwanamuziki maarufu na mkongwe nchini, Kikumbi Mwanza Mpango Mwema, maarufu kama King Kiki na kuzikwa siku hiyo hiyo kwenye Makaburi ya Kinondoni.
Mwanamuziki huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 15, nyumbani kwake Mtoni kwa Aziz Ally, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mtoto wake, Jesca Kikumbi, mwanamuziki hiyo alikuwa akisumbuliwa na tezi dume, pia saratani ilikuwa imepanda hadi kwenye ini.
Kwa msaada wa Serikali, King Kiki, alipelekwa nchini India kwa matibabu, na alikuwa kitandani kwa kipindi kirefu akiugua.
KING KIKI NI NANI?
Ni mwanamuziki, mwimbaji na mtunzi mahiri nchini, aliyekonga nyoyo za Watanzania wengi wa rika mbalimbali kuanzia watu wazima hadi watoto.
Nikisema hivyo ni kwamba watu wazima wanamfahamu kwa nyimbo zake alizotunga na kuimba akiwa na bendi ya Orchetra Fauvette, baadaye Maquis du Zaire, Orchestra Safari Sound, 'Masantula Ngoma ya Mpwita', Orchestra King Kiki Double O, Sambulumaa, Zaita Musica na Ya Capital, Wazee Sugu.
Vijana wa sasa wanamkumbuka mzee Kiki kwa ngoma yake inayochengua sehemu zote za burudani, 'Nzibola', lakini wenye wakiitambia kwa jina la 'Kitambaa Cheupe'.
KUINGIA NCHINI
Alizaliwa Januari Mosi, 1947, Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, baadaye akaondokea kuwa mwanamuziki maarufu hasa nchini akiwa na bendi mbalimbali.
Mara ya kwanza alifika nchini Tanzania akiwa na bendi ya Orchetra Fauvette mwanzoni mwa miaka ya 1970, akiwa na Freddy Ndala Kasheba na kutoa vibao mbalimbali kama 'Vivi', 'Nono na Kalimie', 'Zula' 'Jackline', lakini alirejea tena Zaire (sasa DRC), ambapo alikuja tena nchini katikati ya miaka hiyo, akijiunga na Maquis du Zaire, akatunga nyimbo nyingi kama 'Kasongo rudi Nyumbani', 'Maggie', 'Nimepigwa Ngwala'.
Alipata umaarufu mkubwa akiwa na bendi hiyo kiasi cha mashabiki kumpachika jina la King, yaani mfalme kutokana na tabia yake wakati huo ya akiwa anaingia ukumbini alikuwa amevaa joho kama refu kama mfalme, lakini pia anapoingia ukumbi mzima unasimama kwa ajili ya heshima yake kama mfalme mpaka anapopanda jukwaani ndipo kila mmoja ataendelea na shughuli yake.
Baada ya kupata umaarufu mkubwa akiwa na bendi hiyo, mfanyabiashara Hugho Kisima, ambaye alikuwa na bendi ndogo wakati huo, Orchestra Safari Sound ikitumia mtindo wa Nyekese, aliamua kuiboresha bendi yake kwa kujaribu kumnyakua.
ANUNULIWA BENZ
Haikuwa kazi ndogo kumshawishi kutoka Maquis du Zaire, hivyo moja ya vishawiki ilikuwa ni kumnunulia gari aina ya Mercedes-Benz ya kisasa wakati huo, iliyomfanya kujiunga na Orchestra Safari Sound (OSS), mwanzoni mwa miaka ya 1980, na akaleta mtindo wa Masantula Ngoma ya Mpwita, uliovuma kweli kweli na kukonga nyoyo ya mashabiki, akitunga na kuimba nyimbo kama 'Ni kweli', 'Mtoto wa Mjini', 'Haruna Kaka', 'Mwaka wa Watoto' na nyinginezo. King Kiki akawa mwamuziki wa kwanza Tanzania kumiliki aina hiyo ya gari, rekodi ambayo hadi sasa sijui kama imevunjwa au la.
Hata hivyo, mkataba wake wa miaka miwili ulikwisha na hakuongezewa tena, badala yake mwanamuziki mwenzake aliyekuwa naye kwenye bendi ya Orchetra Fauvette, Ndala Kasheba, anaja kuiongoza bendi hiyo na kuanzisha mtindo mpya wa Dukuduku, badala ya ule wake wa mwanzo, Masantula.
King Kiki alirejea nyumbani, Maquis, ambayo kwa wakati huo sasa ilibadilishwa jina la kuitwa Maquis Original, ambapo alitunga nyimbo kadhaa, lakini kuna zingine aliziimba kwa istadi mkubwa kama 'Double Double', 'Malokelee', na 'Anjelu.'
KING KIKI DOUBLE O
Aliondoka tena Maquis na kuanzisha bendi yake aliyoiita Orchestra King Kiki Double O, mwanzoni mwa miaka ya katikati na mwishoni mwa miaka ya 1980, akipata msaada wa vyombo vya muziki kutoka kwa mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu wakati huo Dk Alex Khalid.
Alianzisha mtindo uliopendwa sana wa Embalasasa, Embalastop, Embala-shika breki, akitunga nyimbo zilizowachengua mashabiki wengi kama vile, 'Kitoto Kaanza Tambaa', 'Malalamiko', 'Dodom Capital', 'Lamanda', 'Pilikapilika Mtaa wa Samora' na nyingine nyingi, baadaye alikuwa mmoja wa waasisi na bendi y Sambulumaa ingawa hakukaa sana
KITAMBAA CHEUPE
Miaka ya 1990 aliungana tena na Kasheba na kuunda bendi ya Zaita Musica moja ya wimbo maarufu ni 'Kesi ya Khanga', baadaye bendi hiyo ilibadilishwa jina la kuitwa Ya Capital 'Wazee Sugu' ambapo ilifanya safari nchini Uingereza ambako ndiko walikokwenda kurekodi wimbo maarufu wa 'Nzibola', mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambao umetokea kupendwa mno na kizazi cha sasa wakiuita, 'Kitambaa Cheupe.' Buriani Maestro King Kiki.
Tuma meseji 0716 350534
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED