TIRA kutumia Sabasaba kutoa elimu Bima ya Afya kwa Wote

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:30 AM Jun 29 2024
Kaimu kamishna bima kutoka TIRA Zacharia Muyengi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu kamishna bima kutoka TIRA Zacharia Muyengi.

MAMLAKA ya Bima Tanzania (TIRA) imepanga kutumia Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara, maarufu Sabasaba, kuelimisha wananchi kuhusu Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Pia imejipanga kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kukata bima ili ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wawe na uelewa wa huduma hizo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TIRA, Zakaria Muyengi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za bima zitakazopatikana wakati wa maonesho ya Sabasaba mwaka huu.

Alisema mamlaka hiyo ina wataalamu wa bima mbalimbali pamoja na wadau wake ambazo ni kampuni 40 zinazotoa huduma hizo ambao wamejipanga kuelimisha wananchi.

"Tunataka tuongeze uelewa na umuhimu wa bima kwa Watanzania kutoka asilimia 20 hadi 25 ya wenye bima sasa hadi asilimia 50 mwaka 2030," alifafanua Muyengi.

Kaimu Mkurugenzi huyo aliomba wananchi kujitokeza kupata elimu hiyo na kwamba wenye migogoro au madai kwa kampuni za bima watahudumiwa pia.

"Msuluhishi wa migogoro ya bima yupo hapa, mwananchi yeyote mwenye tatizo aje amwone ili shida yake itatuliwe," alisema.

Ofisa Mtendaji wa Muungano wa Kampuni za Bima, Elia Kajiba, alisema wananchi wenye madai mbalimbali watapatiwa huduma wakati wote wa maonesho.

"Bima ni rafiki wa jamii kuanzia afya, makazi, kilimo, biashara na maisha kwa ujumla kwa sababu inakukinga dhidi ya majanga mbalimbali. 

"Tunawaalika wananchi wa Dar es Salaam na mikoa jirani waje wapate huduma, hata wale wenye madai hapa ni mahali sahihi kuja," alisema.

"Una madai yako unafuatilia, hapa ni mahala sahihi pa kupata mrejesho. Kama una mgogoro na kampuni yoyote, hapa ni sehemu sahihi kabisa," alisema Kajiba.

Serikali imekusudia kutumia mapato yatokanayo na pombe kali, vinywaji baridi, vipodozi na kamari, kuhudumia Bima ya Afya kwa Wote kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024.