MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) "hakitatoboa" katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Akizungumza jana na wananchi wa Dareda, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, Mbowe alisema, "Ninawahakikishia mwaka ujao (wakati wa Uchaguzi Mkuu) ndio mwisho wa CCM. Uchaguzi huru na wa haki hawawezi kutoboa.
"Tunatafuta tena nguvu tuinyanyue CHADEMA kule ilikokuwa, iweze kuwa sauti ya wananchi. Uchaguzi wa vijiji na mitaa mwaka huu, Kata nzima ya Dareda na kata jirani, tukawafundishe CCM kwamba wameshaishiwa nguvu, hawana uwezo wa kushinda. Sisi tutashinda kwa mapenzi ya wananchi, kwa sababu Mungu yuko upande wa wale wanaoitafuta haki.
"Tunasema angalao tupite kata kwa kata kadri iwezekanavyo, tuwasalimie wananchi tuwatie moyo, msikate tamaa mambo mazuri yanakuja."
Mbowe alisema wanakwenda kushindana na CCM huku akiwaaminisha wananchi kwamba mwaka ujao kuna uwezekano mkubwa kuwa ndiyo mwisho wa CCM kuongoza nchi.
Akiwa Dareda, Mbowe aliwataka wakazi wa eneo hilo kuhakikisha wanarejesha wabunge na madiwani wa CHADEMA.
ULEVI KWA VIJANA
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini na Mbunge wa zamani wa Arusha, Godbless Lema, akiwa Haydom, Dongobesh, Katesh na Dareda, alisisitiza kwamba hivi sasa kuna tatizo la ulevi wa kupindukia linaloitesa nchi.
Lema alisema tatizo hilo limesababisha vijana wadogo wenye umri kati ya miaka 20 na 40 kuwa wagonjwa wa figo.
"Leo vijana wadogo ndio wagonjwa wa figo ambao ni kati ya miaka 20 na 40. Hii ni kwa sababu ya pombe kali. Umasikini umewafanya wakapoteza matumaini, wakawa walevi, wanakula dawa za kulevya.
"Tunaongea kwa ajili ya watoto hawa kwa kuwa watakuja kuyachapa fimbo makaburi yetu kwa kushindwa kuona nchi inaharibika. Watu leo ni masikini, hali mbaya, vijana wote wameishia kuwa madereva bodaboda, hakuna viwanda, hakuna mashamba, hakuna uchumi.
"Dada zetu wanakwenda mjini kuwa ‘... (alitaja neno lenye maana ya biashara haramu), hali ni mbaya, wote hapa mmevaa mitumba, mnajitia moyo, huo ni umasikini. Tunaagiza chumvi nje ya nchi kati ya Sh. bilioni 20 hadi Sh. bilioni 30 wakati Bashnet kuna chumvi," alisema.
Lema alishauri serikali kufikiria kufungua kiwanda cha chumvi Bashnet ili kuzuia chumvi ya nje ya nchi kuingia kwa kuwa kufanya hivyo katika Mkoa wa Manyara kutatoa ajira kwa wananchi wake.
Kuhusu mchele, Lema alisema mchele wa Magugu ni bora duniani, lakini unaishia Arusha na Dar es Salaam.
"Ukichukua mchele wa Magugu leo ukaupeleka Marekani, kilogramu moja ni Dola nane, Dola 10. Dola 10 ya Marekani, ni karibu 25,000 ya Tanzania.
"Maana yake gunia la kilogramu 100 utauza Marekani milioni 2.5. Serikali ingeenda kwa wakulima wa Magugu, ingewaambia chukueni mitaji hii, lima mashamba laki moja (100,000), laki mbil (200,000i, laki tatu (300,000).
"Weka kiwanda cha kupaki mchele, weka track (malori) ya kupeleka mchele Arusha, weka kwenye treni peleka Tanga-Bandarini, peleka Marekani.
"Mchele ambao mpaka umetoka shambani umetumia Sh. 1,000 kwa kilogramu. Vijana wote wangeajiriwa na kujiajiri mashambani, wangepewa mikopo na wangelipa bima ya afya kwa wote na familia zao 'zingekula bata'," alisema Lema huku akishangiliwa na wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED