Vilevi, vipodozi na kubeti vyapingwa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:13 AM Jun 28 2024
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.
Picha: Maktaba
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

MBUNGE wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu (CCM) amesema hakubaliani na Wizara ya Fedha kupendekeza vinywaji baridi, pombe kali, vipodozi pamoja na kamari kutumika kama vyanzo vya mapato kwa ajili ya kuhudumia Bima ya Afya kwa Wote.

Jesca ametoa kauli hiyo bungeni wakati akichangia mjadala wa muswada wa Fedha wa mwaka 2024 ulisomwa kwa mara ya pili na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Amesema si jambo zuri kwa kinamama wajawazito na watoto kupatiwa matibabu yao kwa fedha zitokanazo na walevi, hivyo serikali inapaswa kutafuta chanzo kingine cha uhakika.

"Haiwezekani leo hii tutegemee pombe, sigara, soda na vipodozi kwa ajili ya kuhudumia matibabu ya watoto wetu, wazee wetu watibiwe kwa fedha za walevi kweli au wachezakamari, hii haiwezekani!

"Chanzo hiki si ‘reliable’ (cha kuaminika) viongozi tafuteni chanzo kingine. Kweli leo hii Bima ya Afya kutegemea fedha za walevi au kinamama wanaojipodoa, si kweli!" Jesca amelalama.

Kutokana na hoja hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu, alisimama na kuomba kutoa taarifa, alipopata rukhsa ya Spika, amesema lengo la serikali kutoza kodi kwa bidhaa hizo ni kupunguza matumizi ya bidhaa hizo kwa wananchi wake.

"Mheshimiwa Spika, viwango vya hizi bima za afya katika maeneo mengi vinatokana na tozo za kodi za bidhaa hizi ambazo zinahatarisha afya za watumiaji ili kiasi kile kinachotozwa kinakwenda kutibu watu," amesema waziri huyo.

Baada ya Dk. Mwigulu kutoa taarifa hiyo, Spika Dk. Tulia Ackson amemwuliza mbunge huyo kama anapokea taarifa hiyo; naye alisema anaipokea lakini akasisitiza serikali itafute chanzo kingine chenye uhakika kwa ajili ya kuhudumia Bima ya Afya kwa Wote.

"Ninaipokea taarifa lakini kama alivyosema, wanatoza kodi ili kupunguza matumizi ya bidhaa hizo na kama kweli watu hawatatumia, maana yake fedha hazitakuwapo kuhudumia Bima ya Afya kwa Wote. Kwahiyo, chanzo hiki kimewekwa tu lakini pia sisi kutumia fedha za walevi kutibiwa haileti picha nzuri," amesema.

KODI YA GESI

Naye Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege (CCM), akichangia mjadala huo, amesema mpango wa serikali kutoza Sh. 382 kwa kilo moja ya gesi asilia unarudisha nyuma jitihada za nchi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.

Kandege amesema matumizi ya gesi asilia yatakuwa na manufaa kwa taifa, hivyo kuweka ushuru huo ni kurudisha nyuma jitihada za serikali.

"Gesi asilia ambayo tutahamasisha wananchi watumie, tunainunua kwa shilingi yetu, hivyo tutaokoa matumizi ya fedha za kigeni ambazo tunatumia hivi sasa kuagiza mafuta nje ya nchi," amesema Kandege.

Mbunge huyo pia ameshauri magari yote ya serikali ambayo yananunuliwa yawe na mifumo miwili ya matumizi ya mafuta na gesi, ili kuhamasisha matumizi hayo na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta.