Mke akitoa siri za ndani jitafakari!

By Flora Wingia , Nipashe
Published at 11:32 AM Jun 30 2024
Mke kutoa siri za ndani.
Picha: Maktaba
Mke kutoa siri za ndani.

MPENZI Msomaji, bado tunaendelea kujadili vituko ndani ya ndoa zetu. Ukiona mwanandoa anatoa siri za ndani, hilo ni tatizo kubwa.

Jamaa mmoja akatuma ujumbe mfupi kupitia simu ya kiganjani akisema: Mimi naitwa Jumanne (jina la pili tunalo), ninapatikana Mlandizi, Pwani.

“Nimeoa mke ila cha ajabu mambo yetu ya ndani huwa anayapeleka kwao, inafikia kipindi mengine yanaleta chuki kwa ndugu zake. Nikimwonya ataomba msamaha. Lakini siku inayofuata atarudia tena, mpaka sasa kumekuwa na chuki kubwa dhidi yangu mpaka ninakosa amani na ndoa yangu. Ninaomba ushauri)”.

Msomaji wangu, nimejaribu kupata maoni toka kwa baadhi ya watu kumshauri jamaa huyu.

Naitwa Alphonce John. Baba huyu ambaye mkewe anaweka mambo ya kifamilia sebuleni (hadharani), afanye yafuatayo ili kutibu hali ya mkewe;

  1.   Yeye mwenyewe baba ajichunguze kasoro zake kiutawala na kiuchumi zinazopelekea mke kutoa siri zao nje.

  2.  Huyu baba ampende mkewe kwa pendo la dhati. Upendo hauhitaji fedha, ni jambo la hulka tu.

  3.  Mipango ya kifamilia aipange mwenyewe asimshirikishe mkewe kwa kipindi cha miezi kadhaa, aongeze utendaji kazi. Mke aone tu anaambiwa kutenda bila kushirikishwa ndio atapata funzo la kuacha kuanika yale ya familia.

Huo ndio ushauri wa msomaji wetu aliompa ndugu yetu huyo kuhusiana na sekeseke hilo. Binafsi nilimshauri mengi ila hapa nikumbushie machache. Kwanza, nilitoa tafsiri ya tabia kama ilivyotoholewa katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la pili la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam.

Tabia: Ni mazoea yanayotokana na kurudiarudia hali, mwenendo au matendo.

Kwa tafsiri hii, ninajaribu kuona ukweli unaojitokeza katika malalamiko ya jamaa hapo juu kwamba tabia ya mkewe ya kutoa habari za ndani ya familia kwa watu wengine imekuwa inajirudiarudia hata pale anapomkanya mara kwa mara.

Baada ya kupata ujumbe wa kijana huyo kupitia simu ya kiganjani, nilimpa ushauri ufuatao; kwamba hiyo ni tabia aliyotoka nayo huko kwao. 

Ndio maana kabla ya kuoa yafaa uchunguze tabia ya mwenzio. Ingawa tabia zingine hujificha au ni vigumu kuzirekebisha kutokana na kujikita kwenye uasili, lakini jitahidi, pambana na ikiwezekana itisha vikao vya ndugu  aonywe, anaweza kubadilika.

Ni ushauri niliompa kwa haraka haraka, lakini bado nilidhani tatizo la bibie huyo lina chimbuko, si bure. Kijana huyu akijaribu kuchimbua uasili wa familia ya mkewe, anaweza kugundua kwamba huenda tabia hiyo ya kuvujisha siri za ndani ya nyumba, amerithi toka kwa mama yake mzazi, au imeanzia kwa bibi mzaa baba au mzaa mama au upande wa baba na kadhalika.

Huo ni mnyororo ambao hauwezi kukatika labda kwa maombi. Na tabia, kwa maandiko ya Mungu ni roho. Ni kitu kinachotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine na kuleta madhara. 

Kwa mfano, kama mama mzazi wa binti alikuwa na tabia hiyo, na binti wakati anakua alikuwa akiona mama yake akifanya vituko kama hivyo, kwanini binti asiviige?

Chanzo cha matatizo wakati mwingine ni wazazi wetu. Kama wazazi hawakuwalea vyema watoto, matokeo yake ndio hayo, huwa mwendelezo wa madhara hata ukubwani. 

Jamaa anasema humkanya mkewe, anaona kabisa amemwelewa lakini baada ya muda hurudia makosa yale yale. Hata yeye mwenyewe (binti) anajishangaa kwanini anarudia aliyokatazwa. Hiyo ni roho inayomfuatilia msichana huyo ambayo inatokana na misingi mibovu aliyokulia.

Hata Mungu ameweka wazi katika moja ya maandiko yake kuhusu misingi kwamba kama haikuwekwa imara, lazima italeta madhara na huwezi kumlaumu mtoto ambaye hukumjenga kitabia.

Anasema; “Misingi ikiharibika, mwenye haki atafanya nini? (Zaburi 11: 3). Mtoto anayo haki ya kuishi maisha mazuri yenye tija. Mzazi ndiye mwenye wajibu wa kumjengea misingi mizuri pamoja na serikali kwa maana ya malezi bora. Sasa kama mtoto hakuandaliwa misingi mizuri ya malezi, akiharibika kitabia, nani wa kulaumiwa?

Msomaji wangu, kabla ya kuoa au kuolewa kwenye familia fulani, chunguza kwanza.  Mfano, tabia; je, ni familia ya aina gani? Wacha Mungu, walevi, waabudu matambiko, washirikina, wambeya, wahuni, waasherati, wafitini, wana wivu, wapole na kadhalika. 

Je, una jambo la kimaisha linakutatiza? Tuma ujumbe mfupi 0715268581, pia ipo WhatsApp Au Email: [email protected]