Wahitaji Zanzibar waelekea kuwa mfano wa kuigwa kimafanikio kijamii, kiuchumi

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:51 AM Jul 02 2024
Wanavikundi vya watu wenye ulemavu vya kuweka na kukopa wakiwa katika vikao vinavyofanyika  kila wiki.
PICHA:RAHMA SULEIMAN.
Wanavikundi vya watu wenye ulemavu vya kuweka na kukopa wakiwa katika vikao vinavyofanyika kila wiki.

TANZANIA imesaini na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu unaozitaka nchi wanachama kuondoa ubaguzi kwa misingi ya ulemavu maeneo ya ajira.

Mkataba unaeleza kuwa wenye ulemavu wana haki ya kufanya kazi sawa na watu wengine.

Licha ya hatua mbalimbali kuchukuliwa kulinda wanaoishi na ulemavu, kama kutunga sheria ya watu wenye ulemavu na kuwawezesha kwa mikopo ya halmashauri changamoto zinaendelea kuwakabili na wana vikwazo vingi mbele yao.

Vikwazo hivyo ni hali ngumu ya maisha, kukosa mitaji ya kufanya biashara, kukosa elimu ya ujasiriamali na kukosa mikopo dhana ambayo sio sahihi ya kwamba hawakopesheki.

 Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) - Zanzibar kwa kushirikiana na shirikisho la Watu Wenyeulemavu Zanzibar (SHIJIWAZA), wanaleta ukombozi kwa kundi la wenye mahitaji maalumu. 

Wanashirikiana kwenye mradi wa Kijaluba, unaowakusanya  wenyeulemavu na kuwapa elimu ya ujasiriamali ili kuachana na hali ya utegemezi.

Mratibu wa Kijaluba Khairat Haji, anasema baada ya kuwapa elimu ya ujasiriamali waliwashajihisha kuunda vikundi vya kuweka na kukopa ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na kuweza kujitegemea.

Aidha, hatua ya kuamua kuvisaidia vikundi hivyo ni kuunga mkono mikakati ya serikali katika kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuwapatia mitaji ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Khairat anawataka viongozi na wanachama wa vikundi hivyo, kuyafanyia kazi maelekezo ya kitaalamu wanayopewa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuanzishwa kwa vikundi hivyo.

“Hivi sasa tunakamilisha mwaka mmoja tangu mradi huo kuanza kuwasaidia watu wenye ulemavu na kuwafundisha kujua haki zao, elimu ya kuweka na kukopa, umuhimu wa kuweka akiba, kutengeneza sabuni, mikoba, ukulima wa mboga na biashara ndogondogo,” anasema.

Lengo limefikiwa kwa sababu mwanzo ilikuwa ni ngumu kutokana na jamii kuwa na mitazamo hasi ya kwamba watu wenye ulemavu ni wa kupewa badala ya kutafuta, lakini  wamehamasika kufanya biashara na kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, anasema.

Aidha, anaeleza kuwa wanufaika wamejengewa uwezo wa kujua, umuhimu wa kuweka akiba, jinsi ya kutumia mikopo, elimu ya biashara na mbinu za kuendesha biashara kulingana na hali zao.

"Tumetoa mafunzo mbalimbali kujua haki zao, umuhimu wa kuweka na kukopa na jinsi ya kutumia mikopo na kufanya biashara na kuziendesha,"anaeleza Khayrat Haji, Ofisa Msaidizi wa Mradi wa Kijaluba.

Anaongeza, “Lengo kuu la mradi limefanikiwa kwa sababu haikuwa rahisi kubadilisha mitazamo iliyojengeka katika jamii kwamba wenye ulemavu ni wa kupokea zaidi misaada badala ya kujishughulisha na kujiongezea kipato”.

Ofisa mwezeshaji wa vikundi vya kijaluba Muhidin Ramadhani, anasema wameweka utaratibu wa kukutana na wanavikundi hao kila muda ili kubadilisha mawazo na kubaini matatizo yaliyopo na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.

Anasema wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kwa sababu mradi huo umepelekea kuimarika kwa watu wenye ulemavu na kupiga hatua kimaendeleo na kufikia malengo ya kujikwamua na tatizo la umasikini.

Muhidin anasema mradi unaendelea na kuvisajili vikundi vilivyopo chini ya mradi huo kupitia Idara ya Ushirika ili vitambulike kisheria.

“Lengo la kuvisajili ni kupata fursa ya kufungua akaunti benki na kutunza fedha katika mazingira bora na salama,” anaeleza Muhidin.

Ramadhani Haji, Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika Tutambuwane kutoka kijiji cha Bwejuu Kusini Unguja, anaeleza kuwepo mradi umewasaidia watu wenye ulemavu kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili wao wenyewe ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto na kuhudumia matibabu ya wagonjwa.

“Kupitia mfuko wa jamii, fedha zetu tunazoweka tumetatua matatizo mbalimbali. Tulipata maafa baadhi ya nyumba zetu kuingia maji na tukapata mkopo, pia wagonjwa waliolazwa walifaidika na mkopo huo kupitia jamaa zao waliojiunga kwenye vikundi," alisema.

Anafahamisha kwamba mradi umeandaa mwongozo maalum wa utekelezaji katika kusimamia uendeshaji wa vikundi vya hisa kwa lengo la kuongeza ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kiuchumi kwenye jamii.

“Ili  kuongeza ujumuishi unaolenga kuwawezesha wenye ulemavu kiuchumi, mradi umeandaa mwongozo unaweka mazingira rafiki ya kukuza uwezo wa watu wenye ulemavu kiuchumi kwa kujenga mitazamo chanya juu ya ushiriki wao na kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato kupitia vikundi vya kuweka na kukopa,” anasema.

Anasema ili malengo hayo yafikiwe ni lazima walimu na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu kutumia mwongozo kusimamia na kuwaelimisha watu hao umuhimu wa ushiriki wao katika shughuli za kujipatia kipato bila kujali hali za ulemavu wao.

Fatma Abrahman mwalimu wa vikundi anawataka walimu kushughulikia changamoto za wenye ulemavu bila kukata tamaa kulingana na hali za ulemavu ili kusaidia kujenga mitazamo chanya ya ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

“Walimu wa vikundi tunatakiwa tusikubali kushindwa na kukata tamaa katika kuwasimamia watu wenye ulemavu. Tuwaongoze kutokana na uhalisia na utaalamu wetu ili tuwasaidie kufikia maelengo na kuwawezesha watu kiuchumi kupitia vikundi vya hisa,” Fatma Abrahman.

Asha Haji Awesu, katibu wa kikundi cha mwanzo mgumu cha watu wenyeulemavu katika Kijiji cha Michamvi, mkoa wa Kusini Unguja, anasema wamefarajika kuanzishwa kwa vikundi hivyo kwasababu vimewasadia kupata mahitaji muhimu ikiwemo kulipia ada za shule kwa watoto wao.

Alisema mradi wa kijaluba umewapatia elimu ya ujasiriamali unaowawesha kuibua miradi mbalimbali ikiwamo kutengeneza sabuni, achari na vipodozi na  mafuta.

Aidha anasema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa mikopo kwa taasisi zinazotoa mikopo zikiwamo benki pamoja na soka la uhakika la kuuza bidhaa.