Diarra, Mustafa wabakia Tanzania

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:22 AM Jul 04 2024
Djugui Diarra.
Picha: Mtandao
Djugui Diarra.

UONGOZI wa Yanga umefanikiwa kumbakisha kipa wake chaguo la kwanza, Djugui Diarra, kwa kumpa mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kuwatumikia mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.

Diarra, ambaye ni golikipa chaguo la kwanza la Timu ya Taifa ya Mali, amesaini mkataba utakaomweka klabuni hapo hadi  mwaka 2026.

Baada ya majadiliano na uongozi wa Yanga kufikia pazuri, Diarra amekubali kuendelea kuitumikia timu hiyo huku akizifungia 'macho' ofa kutoka katika klabu nyingine zilizokuwa zinataka huduma yake.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema jijini Dar es Salaam jana uongozi wao uko makini katika mchakato wa usajili wa wachezaji kwa kuhakikisha inawabakisha nyota wote inaowahitaji.

Kamwe alisema chini ya Rais Hersi Said, Yanga imedhamiria kuona timu yao inaendelea kufanya vizuri katika msimu mpya wa mashindano ya ndani na ya kimataifa.

“Tunataka msimu ujao kufanya vizuri zaidi, kuanzia katika mashindano ya ndani na Klabu Bingwa Afrika, tunataka tufike mbali zaidi ya msimu huu ulioisha,” alisema Kamwe.

Aliongeza Diarra amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha timu hiyo na amechangia mafanikio waliyoyapata katika kipindi chote tangu ajiunge na mabingwa hao.

“Lengo letu ni kuona tunafanya vizuri zaidi ya msimu uliopita katika mashindano yote, kwa hiyo uongozi hautamwacha mchezaji tunayemhitaji aondoke kwenye kikosi,” Kamwe alisema.

Wakati huo huo, Azam FC, imempa mkataba wa miaka miwili golikipa wake namba moja, Muhamad Mustafa, ambaye ni raia wa Sudan.

"Muhamad bado yupo hapa," ilisema taarifa rasmi iliyoandikwa na klabu hiyo ya Chamazi.

Mustafa, ambaye ni kipa chaguo la kwanza wa Timu ya Taifa ya Sudan, alikuwa akiitumikia Azam kwa mkataba wa mkopo akitokea El Merreikh.