Chama: ‘Thank you’ Simba

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 08:16 AM Jul 04 2024
Clatous Chama.
Picha: Mtandao
Clatous Chama.

WAKATI ikiendelea kushusha vifaa vipya kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake, aliyekuwa kiungo wa kimataifa wa Simba kutoka Zambia, Clatous Chama 'Mwamba', rasmi amewaaga mashabiki na wanachama wa Wekundu wa Msimbazi huku akisema historia haitabadilika.

Yanga ilitangaza kumsajili Chama mapema wiki hii ikiwa ni baada ya mkataba wa Simba na Mzambia huyo kumalizika Juni 30, mwaka huu.

Nyota huyo jana aliandika pia katika ukurasa wake wa Instagram yeye ni mchezaji wa Yanga na Timu ya Taifa ya Zambia maarufu Chipolopolo.

Chama ambaye alijiunga na Simba akitokea Lusaka Dynamo FC ya Zambia alisema jana alikuwa na miaka sita yenye furaha, mafanikio na changamoto mbalimbali.

Kiungo huyo aliyetua Simba mwaka 2018, halafu miaka mitatu aliuzwa katika klabu ya RS Berkane ya Morocco na baadaye kurejea kwa Wekundu wa Msimbazi alisema alifanya kazi yake Simba kwa upendo na alipata heshima kutoka kwa wachezaji, viongozi na mashabiki.

“Miaka sita iliyopita nilikuja kama mgeni. Mlinipa malengo na changamoto za kunifanya kuwa bora zaidi. Sina la ziada zaidi ya heshima kwa kila mmoja wenu kwa upendo na ushirikiano mlionipa kwa miaka yote, hakuna anayeweza kubadilisha historia tuliyoitengeneza pamoja.

Nawatakia kila la kheri na tuendelee kuonana katika nyakati nzuri,” alimaliza Chama ambaye ana umri wa miaka 33.

Hata hivyo Chama ambaye ni mmoja wa wachezaji nyota katika kikosi cha Chipolipolo, utambulisho wake wa kujiunga na Yanga haujafanana na thamani aliyonayo.

Simba ilifikia uamuzi wa kutompa kiasi cha fedha ambazo alikihitaji kwa kuzingatia umri na kiwango alichokionyesha katika mwaka wake wa mwisho wa mkataba.

Ubora wa Chama ambaye amezaliwa kwenye familia ya wanasoka ulianza kuonekana alipokuwa akiitumikia ZESCO United ya Zambia ambapo mwaka 2016 alionyesha kiwango cha juu na kusajiliwa na Al Ittihad ya Mısri mwaka 2017 ingawa alicheza kwa muda mfupi na kurejea kwao Zambia.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili mabosi wa klabu hiyo wanaendelea kufanya usajili bora ambao utawafikisha katika malengo yao kwenye mashindano yote watakayoshiriki msimu ujao.

Ahmed alisema wamefahamu walipokosea na sasa wanajiimarisha katika kila idara ili kurejesha heshima na furaha kwa mashabiki na wanachama wa Wekundu wa Msimbazi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, alisema bado hawajamaliza mchakato wa kusajili wachezaji wapya.

"Familia inazidi kuongezeka, napenda kuwaambia kila mchezaji ambaye tutamtangaza ni mchezaji mwenye rekodi, anayekuja kutupeleka katika malengo yetu, tutakuwa moto, tumejenga kikosi imara," Kajula aliongeza.

Juzi Simba ilitangaza kukamilisha usajili wa Joshua Mutale kutoka Zambia na Steven Mukwala, ambaye ni nyota wa Timu ya Taifa ya Uganda (Uganda Cranes), aliyekuwa akiitumikia Asante Kotoko ya Ghana.

Hata hivyo bado Simba bado haijatangaza kocha mkuu mpya ambaye anakuja kurithi mikoba iliyoachwa na Mwarabu wa Algeria, Abdelhak Benchikha.