Aussems aitabiria mazuri Singida BS Ligi Kuu Bara

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:29 AM Jul 04 2024
Kocha Mkuu, Patrick Aussems
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu, Patrick Aussems

SIKU moja baada ya kuwasili nchini na kusaini mkataba wa kuifundisha Singida Black Stars, Kocha Mkuu, Patrick Aussems, amesema timu hiyo itakuwa miongoni mwa timu zinazocheza soka safi la kuvutia.

Aussems, kocha wa zamani wa Simba, amesema hawezi kuahidi kikosi hicho kitachukua ubingwa lakini anaamini baada ya miaka michache Singida Black Stars itakuwa klabu bora hapa Tanzania.

"Nilikuwa na hapa nikiifundisha Simba, tuliijenga timu na kuanza kufanya vizuri na kuwa na jina kubwa, naamini na Singida itakuwa hivyo hivyo," alisema Aussems.

Aliongeza anatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa klabu pamoja na wachezaji.

"Nje ya Tanzania inajulikana zaidi klabu ya Simba na Yanga kidogo, hii ni nafasi ya kuiandaa Singida ili kuwa miongoni mwa timu bora hapa Tanzania, hilo linawezekana kwa ushirikiano wa watu wote, benchi la ufundi, wachezaji na viongozi," alisema Aussems.

Kocha huyo alisema anajua Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa na ushindani na hiyo inasaidia kukuza soka la hapa nchini.

"Nimejiandaa kukabiliana na ushindani kutoka kwa kila timu inayoshiriki Ligi Kuu, hakuna mechi rahisi, hakuna tena timu ndogo," Aussems alisema.

Wakati huo huo mabosi wa timu hiyo wameomba kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini hivi karibuni.