DK NEVER MWAMBELA: Mgunduzi dawa isiyo na kemikali,kutibu mazao

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 07:45 AM Jul 02 2024
news
Picha:Mpigapicha Wetu
Mbunifu wa kiuatilifu vuruga Dk.Never Mwambela.

BAADA ya kuhitimu shahada ya uzamivu katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela-Arusha, Dk. Never Mwambela, anaandika historia Tanzania na Afrika pia.

Ni ya ugunduzi wa kwanza unaofanywa na mwanamke Tanzania na Afrika, akibuni kiuatilifu hai kisicho cha kemikali kinachotumika kudhibiti visumbufu kama kantangaze kwenye nyanya, viwavijeshi vinavyoharibu mahindi na viwavi vitumba jamii ya wadudu waharibifu kwenye pamba.

Amefanya shahada ya uzamivu (PhD) kwenye kantangaze na kugundua kiutilifu kinachoitwa ‘Vuruga Biocide.’ Ni kiuatilifu hai (hakina sumu wala kemikali), lakini hakuishia hapo ameanzisha kampuni ya Plant Biodefenders mwaka 2019 na kusajili kiuatilifu hicho kinachotumika nchini na juhudi za kukisambaza Afrika zikiendelea.

KANTANGAZE NININI? 

Mtafiti huyu anapozungumza na Nipashe, anaeleza kuwa kantangaze’ ni wadudu vamizi waliotokea Amerika ya Kusini tangu mwaka 1914 na kusambaa Ulaya miaka ya 2000 na hatimaye Tanzania 2014 wakionekana kwanza eneo la Ngarenanyuki mkoani Arusha na sehemu nyinginezo.

“Ni mdudu mdogo sana lakini ana athari kubwa anashambualia hatua zote za mmea kuanzia miche, majani, shina, maua na matunda ya mazao jamii ya nyanya ikiwamo nyanya zenyewe, pilipili hoho, nyanya chaungua na mboga ukiwamo mnavu”

Pia anaharibu  pipipili zote, biringanya na magugu yenye jamii ya nyanya kama ndulele hivyo kusambaa kwa haraka hasa wakati wa kiangazi na joto.” Anaongeza.

Anasema PhD yake, imefanyika kwenye vivamizi hivyo ambavyo hushambulia kwa kasi mahindi na kwamba, alianza kukizalisha kiutalifu cha kupambana na mdudu huyo katika maabara ndogo iliyotengeneza lita 100 za dawa kwa wiki wakati wa usajili mwaka 2020.

Mhadhiri huyu mwandamizi na Meneja wa Taaluma wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika-Mweka, mkoani Kilimanjaro, pia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Plant Biodefenders, anayoimiliki.

Akizungumzia mafanikio ya ubunifu wake anasema:“Kwasasa kampuni imejenga kiwanda chenye thamani ya Sh.milioni 680 na imeajiri wafanyakazi 12 wa kudumu na watatu wa mkataba na ajira za muda mfupi na vibarua 20 pia wapo.”

Anaeleza kuwa kiwanda hicho kipo Shirimatunda mkoani Kilimanjaro, na kwamba ujenzi hadi Disemba 2023 uligharamu Sh 680,000,000 na wadau kadhaa wanahusika na uwekezaji huo.

Anawataja kuwa ni pamoja na yeye mwekezaji na mdau mkuu, wanahisa, serikali, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), UDPF-UNCDF, KFW-DeveloPPP ( ya Ujerumani) kupitia  Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU).

 “Tumetengeneza ajira nyingine pia kupitia mawakala wa viuatilifu katika mikoa mbalimbali na tunaendelea kuajiri vijana wengi na wanawake kwa kuwa kiuatilifu hakina athari za kiafya hivyo kuwavutia vijana zaidi.” Anaongeza:

Aidha, anasema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha lita 1,000 za kiuatilifu hai kwa siku zinazoweza kunyunyiziwa kwenye heka 8,000 za mashamba kwa siku, hivyo kutoa mchango mkubwa wa kupunguza tatizo la upungufu wa viuatilifu pia matumizi ya kemikali za sumu zinaoathiri ikolojia.

Anasema :“Pamoja na hayo hiki ni kiwanda cha kwanza na cha kipekee nchini na Afrika kwenye kutengeneza viuatilifu hai. Kimesajiliwa kina haki miliki namba Africa Regional patent No. AP/P/2019/01149. Kinatambulikwa kuwa kinachozalisha kiuatilifu chenye ufanisi katika maeneo matatu kwa wakati mmoja.”

UFANISI WA VURUGA

Anaeleza kuwa ni kuua visumbufu kwa asilimia 80 mpaka 100, kurutubisha mimea, kupunguza matumizi ya mbolea na huvutia wadudu rafiki kama nyuki ili kuongeza uchavushaji na mavuno pia huku kikipunguza gharama za uzalishaji.

Anasema :“Kwasasa kampuni imewafikia wakulima zaidi ya 9,000 pekee japo idadi ni kubwa zaidi. Kimeokoa zaidi ya eka 72,000 za mazao kwa mwaka ambao ni wateja wa kudumu wanaolima mahindi, nyanya na pamba.”

Dk. Never anasema kwenye mahindi vuruga  imenusuru heka 3,200, nyanya 4,000, pamba 4,500, mboga na parachichi heka 300 katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Kilimanjaro, Tanga, Mwanza, Arusha, Morogoro, Tabora, Pwani, Dar es salaam, Iringa, Njombe, Unguja, Zanzibar, Mbeya na Manyara.

Pamoja na mafanikio hayo, baada ya kujenga kiwanda hicho anasema kampuni yake imepunguza bei za kiuatilifu kwa asilimia 10 ili kuwawezesha wakulima kumudu zaidi na kuepuka hasara hasa kwenye mahindi ambako viwavi jeshi vamizi vinaleta uharibifu mkubwa na kusababisha upotevu wa chakula pamoja na hasara kwa mkulima.

Anasema:“ Pia kampuni ipo katika hatua za kusajili viuatilifu vingine hai na mbolea za asili ili kuleta tija katika sekta ya kilimo na kupunguza matumizi ya kemikali ambazo zinaathiri bayoanuai na kutishia afya za wanadamu.”

Mtaalamu huyu , anasema kutokana na kiwanda hicho kuhudumia sekta ya kilimo ambayo ina umuhimu wa kipekee kwenye kufikia utoshelevu na usalama wa chakula, kinakusudia kuleta mabadiliko ya kilimo hai na kuongeza tija katika uchumi endelevu kwa kuwalenga vijana na wanawake.

Anaongeza kuwa vuruga haina kemikali wala kiambata sumu, na imetengenezwa kwa kiambata hai fangasi aina ya ‘A.oryzae’ ndicho kinachoua wadudu na kuboresha udongo na mimea.

Kadhalika,haileti usugu kwa wadudu kwakuwa hakuna kiambata kemikali (chemical active ingredient). 

“Kiuatilifu hiki kina mchango mkubwa kwenye ikolojia kwakuwa ni fangasi ambayo inarudisha vimelea na virutubisho kwenye udongo na haina athari kwa viumbe wasiokusudiwa kama nyuki.  

Pia tumefanya majaribiao kwenye pamba mfano mbegu za Afrisian mkoani Simiyu na Shinyanga, kahawa-KPL mkoani Kilimanjaro na mahindi Kibaha mkoani Pwani.”

Anasema taasisi ya Biocontrol inayohusika na kufuatilia na kutafiti matumizi ya viumbe hai kama fangasi, mimea na wadudu, ina ushahidi wa kitafiti uliochapishwa na kuonyesha kuwa vuruga inavutia nyuki na wadudu wengine kama buibui wenye kazi kubwa kwenye ikolojia.

“ Ikutumiwa kwenye nyanya zinazaa sana na kutoa maua mengi na kuvunwa mara nyingi. Katika mahindi yakikatwa kiini na kiwavijeshi ‘Vuruga Biocide’ ni tiba kwakuwa ina kiambata cha kimelea cha asili , kinawezesha kuchipusha upya na mimea ya jamii ya matunda ya miti mfano maembe, machungwa, mapapai yaliyojeruhiwa huchipuka kwa kasi pia.Yote haya tumetafiti na tuna majibu ya kiutafiti.”

Wakulima wengi wanaguswa na suala la bei , anapoulizwa gharama ya kiuatilifu hicho, anasema kuwa lita moja inauzwa Sh.30,000 na ina uwezo wa kunyunyiziwa kwenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya heka sita.

Anasema kuwa wakulima wakinunua watapata maelezo zaidi ya matumizi kwa wauzaji na pia vipeperushi vitawapa uelewa zaidi .

KUTIKISA AFRIKA 

Dk. Never anasema yeye ni mtoto wa Afrika, japo anaanza kwanza kazi nyumbani lakini ana mpango wa kusambaza vuruga kwenye mataifa mengine ya Afrika ili kudhibiti wadudu jamii ya kantangaze.

Anasema visumbufu hivyo vinavyofahamika kitaalamu kama (Tuta absoluta) na viwavijeshi vamizi (fall armyworm) na viwavi wa vitumba vya pamba (boll worm), wadudu wa parachichi (False codling moth)  wapo maeneo mengi ukanda wa Afrika na kwa karne nyingi hawajapata suluhisho.

“Wadudu hawa wamesababisha usugu kwenye viatilifu vya kemikali na kuacha mabaki ya kemikali za sumu kwenye mazao na kukwamisha soko la nje hasa kwenye parachichi. Vuruga biocide ina ufanisi na haiachi mabaki, wala kemikali kwenye chakula hivyo ni salama kwa mlaji na mazingira. 

Anaongeza kuwa wakulima wa pamba wanaoitumia wanasafririsha pamba yao Japan, German na  China bila vikwazo kwakuwa haina mabaki ya sumu.

MBOLEA ZIKO NJIANI

Akizungumzia mbolea za asili, anakiri zipo nchini kutoka kwa wajasiliamali wengi, hivyo kampuni ya  Plant Biodefenders itaongeza nguvu na kwamba wanakuja kusajili aina nyingine.

Anasema mbolea asili zitasajiliwa ili kuzalishwa baada ya utafiti, ambazo anasema zinashika kasi na zitatatua changamoto inayotokana na chumvichumi kuharibu ardhi na kuathiri walaji.

Anasema kwa sasa mbolea za mwani au mazao ya bahari ndiyo tegemeo: “Mbolea inayotokana na mwani ndilo suluhisho la kudumu kwakuwa kilimo cha mwani ni chachu endelevu ukanda wa pwani ya Tanga na Pemba.” 

Anafafanua kuwa kila bidhaa zilizotengenezwa zimetafitiwa, zina haki miliki na hadi sasa ana haki miliki nne za mbolea na zina tuzo za kimataifa na kitaifa.

Dk. Never kuanzia mwaka 2020 ni mhadhiri mwandamizi na Meneja wa Taaluma katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika cha Mweka, akishughulikia kupanga na kuratibu miradi ya ubunifu inayoboresha maisha ya watu.

Kadhalika, anasimamia na kuendeleza uhifadhi wa bayoanuai na teknolojia zinazotunza mazingira kwa uendelevu.