MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewajibu wanasiasa wanaokihama chama hicho na kumshambulia, huku akiwataka Watanzania kutokiangalia chama hicho kwa sura ya Mbowe.
Bila kumtaja mtu, alirusha dongo kwa wanaokitazama kwa sura hiyo, akiwataka wanaomshambulia pamoja na Watanzania wengine kuiangalia CHADEMA kwa mambo inayoyasimamia.
Akizungumza jana na wananchi wa Kabuku, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, anakoendelea na operesheni iliyobatizwa jina la Operesheni GF alisema:
“Chama hiki sio cha Mbowe. Mmejenga chama chenu na chama hiki leo kimekuwa nchi nzima. Samia anajua (Rais Samia Suluhu Hassan), Majaliwa anajua (Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa). Nyie wananchi wa Tanga msikiangalie CHADEMA kwa sura ya Mbowe.
“Kiangalieni CHADEMA kwa mambo ambayo inayokisimamia. Chama hiki kina misingi minne. Msingi wa kwanza, ni haki kwa watu wote, haki kwa watoto, haki kwa wamama, haki kwa wababa, haki ya kuabudu, haki ya kila mmoja aheshimiwe kwa nafasi yake.
…Ndani ya serikali ya CCM, watu wamebanwa kila mahali michango, kila mahali manung’uniko, kila mahali uonevu,kila mahali viposhoposho sijui vimichango michango. Mtendaji wa Kata anakuzonga, Mwenyekiti wa Kijiji anakuzonga, uongo kweli? Tunataka tujenge taifa la watu huru, furaha.”
Akionyesha kuchukizwa na wanaokikosoa kwa kukitazama CHADEMA kwa sura yake, Mbowe, alisema wanapaswa kuutazama msingi wa tatu, ambao ni chama ambacho kina msingi wa kuamini viongozi wa watu wapatikane kwa kura za wengi.
Katika mkutano huo, Mbowe alieleza kushangazwa kwake na mkoa huo wenye neema ya ardhi yenye rutuba wakati wote, watu wake kukabiliwa na umasikini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED