Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema uzinduzi Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ilivyoboreshwa utafanyika Januari 31, mwaka huu jijini Dodoma na imezingatia masuala mbalimbali ikiwamo hoja za wadau kuhusu lugha ya kufundishia na matumizi ya Akili Mnemba.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini humo, Prof. Adolf Mkenda amesema uzinduzi huo utafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na utahudhuriwa na wadau na viongozi takribani 3,000.
Amesema kuna hoja mbalimbali ambazo zinazungumzwa na wadau na wananchi ambazo majibu yake yapo kwenye sera na mitaala hiyo mipya ikiwamo mjadala mkubwa unaoendelea kwa sasa kuhusu somo la Kiingereza.
“Kwenye sera suala la lugha lipo na kwenye mitaala ni ufundishaji wa lugha, pia tunasikia watu wanazungumza suala la Akili Mnemba ni suala kubwa sana ukienda kwenye sera utaona masuala ya Tehama na mambo yote ya Tehama yaliyozungumzwa na ukija kwenye mitaala utaona utekelezaji wake unavyofanyika,”amesema.
Amesema kuna masuala ya kumuandaa mwanafunzi, sio tu kwenye ubora wa elimu lakini kuwa na ujuzi unaomuandaa kwenye dunia ya sasa na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED