Bil. 31/- yakwamisha miradi 724 ya maendeleo Singida

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 08:14 AM Jun 30 2024
Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego.

UJENZI wa miradi 724 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 31 inayotekelezwa mkoani Singida, umekwama kutokana na kuhitaji fedha za ziada.

Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego, ameyasema hayo wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

Halima amesema hatapenda kusikia miradi yoyote ya maendeleo inayoibuliwa katika halmashauri za mkoa huo inakwama kwa kisingizio cha kutaka kuongezewa fedha za ziada.

Amesema kuanzia sasa halmashauri zote zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha miradi yake kwanza ikiwamo maboma yote yaliyojengwa kabla ya kuanzisha miradi mipya.

Mkuu wa Mkoa ameagiza madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji miradi ya maendeleo badala ya wao kuanza kulalamika kuwa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao haikamiliki.

"Madiwani mnatakiwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo katika maeneo yenu na miradi hiyo ilete matokeo chanya kulingana na thamani ya fedha," Mkuu wa Mkoa Halima ameagiza.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, ameelekeza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuwa wabunifu katika utekelezaji miradi ya maendeleo ikiwamo kuajiri kwa mkataba wahandisi waliostaafu na mafundi wenye ujuzi wa kujenga, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wake.

Dk. Fatuma amesema anajua kuna uhaba wa watumishi hasa katika kada ya uhandisi, lakini usiwe kisingizio cha miradi kukwama.

Amesema ni muhimu wakurugenzi wakawa na njia mbadala ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa.

Katibu Tawala amesema miradi yote ya maendeleo ambayo haijakamika lazima iingizwe katika bajeti mpya ili ujenzi wake ukamilike. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega, ameshuruku serikali kwa kuipatia fedha nyingi halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo.

Mkwega amesema tangu aanze kazi ya udiwani hajawahi kuona fedha nyingi zinazotolewa na serikali kama kipindi hiki, hivyo madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha miradi inakuwa na ubora kulingana na thamani ya fedha.