Undani ajali zinazoua ndugu wengi pamoja

By Romana Mallya ,, Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:47 AM Jun 30 2024
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi Ramadhan Ng’azi.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi Ramadhan Ng’azi.

AJALI zinazosababisha vifo vya ndugu wengi kwa wakati mmoja zina madhara makubwa kisaikolojia, wataalamu wamethibisha.

Wameonya kuwa wanaopoteza wapendwa wao kutokana na ajali hizo, wasipopata tiba ya kisaikolojia mapema, wanakuwa katika hatari kupata kiwewe (trauma) na msongo mkubwa wa mawazo, hata kutishia uhai wao.

Ni angalizo linalotolewa na wataalamu hao kipindi ambacho kumekuwa na ajali za barabarani zinazosababisha vifo vya ndugu wanaosafiri pamoja katika maeneo mbalimbali nchini.

Ajali hizo ni pamoja na mwanzoni mwa juma hii (Juni 24) wilayani Korogwe, mkoani Tanga iliyohusisha wanafamilia, wanne wakifariki dunia wakati wakitoka kwenye harusi ya kijana wao jijini Dar es Salaam, wakirejea kwao Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Msaikolojia Tiba kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Isaac Lema, anasema majonzi kwa wale ambao wamepoteza ndugu kwa wakati mmoja katika ajali huwa hayaelezeki na huchangia wahusika kubaki na maswali yasiyo na majibu.

"Kuna lile swali 'imekuaje?' Huja na kiwango cha juu cha msongo kiasi ambacho wengine katika hilo wanapata kipindi kirefu cha kuwa katika hali ya kutokuwa sawa na wasipopatiwa msaada wa karibu msiba huwa mzito.

"Ndio maana misiba ya namna hiyo ambayo hujitokeza katika hali isiyotarajiwa, unakuta faraja yake huwa tofauti, kunakuwa na wingi wa watu. Asipopata faraja kubwa au usaidizi wa kutosheleza inatishia pia uhai wake.

"Ikifika mahali ikatishia maisha yake na kutaka kuwa msongo wa juu, linaanza kugeuka kuwa jeraha la kisaikolojia. 

"Mara nyingi misiba ya namna hii huleta kiwewe na kusababisha kuona wale watu (ndugu) kama wanajitokeza (mbele yao), hivyo jeraha linakuwa kubwa," Lema anasema.

Msaikolojia Tiba huyo anasema wamekuwa wakipokea watu wa namna hiyo na jambo la kwanza katika kuwatibu, hujielekeza kutambua kiwango chao cha msongo, wameathirika kwa kiwango gani.

"Kama ni jeraha tunatibu, kama litahitaji msaada saidizi tunatoa msaada wa kwanza wa kisaikolojia wa kijamii ambao unawajengea uwezo wa kupambana na hiyo hali mapema. Tunapowaona mapema ndio tunazuia madhara makubwa yasijitokeze.

"Wakifika mapema tunawasaidia kuwakinga dhidi ya magonjwa ya akili ambayo yanaweza kujitokeza, mfano, msongo baada ya janga na wakati huohuo tunatengeneza mazingira ya kumsaidia aliye na jeraha apatiwe matibabu, kwa sababu kuna matibabu ya kisaikolojia ya kutibu majeraha hayo," Lema anafafanua.

Mtaalamu huyo anasema wanapotibiwa majeraha hayo, huwa wanasonga mbele, huku wakiendelea kuwafuatilia kwa kuwa huchukua hadi miezi mitatu, sita na wakati mwingine mwaka mzima kutegemeana na uwezo wa mhusika katika kukabiliana na janga hilo.

"Si lazima akubaliane na hali. Unaweza kukubaliana na hali, lakini hujarudi kwenye hali ya kawaida. Mfano, kama amekubaliana na hali lakini hajaweza kuishi pasipo yule mhusika, bado itakuwa changamoto," Lema anasema.

Msaikolojia huyo anatoa wito kwa wote wanaopata changamoto hizo, wapatiwe huduma mapema ili kukingwa dhidi ya magonjwa ya akili yanayoweza kujitokeza kwa kuwa mengi huwapokea wakiwa na msongo mkubwa.

Jambo la pili, Lema anasema kwa wale walioachwa wanapaswa kujengewa uthabiti ili maisha yao yasonge mbele.

Msaikolojia Tiba huyo anashauri watu waepuke kusafiri ndugu wengi kwa chombo. Panapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo, basi kuwe na utii wa sheria za usalama barabarani.

"Ndugu kusafiri katika chombo cha usafiri kimoja huchangiwa na mazingira fulani na wakati mwingine hayawezi kuepukika, hivyo ikitokea hivyo ni muhimu kufuata kanuni na sheria za usalama barabarani na kuvijua vyombo wanavyosafiria vikoje.

"Wapo wengi wanaosafiri katika chombo kimoja kama familia, lakini hawakutani na majanga hayo. Kwanini? Ni kwa sababu wanafuata kanuni na sheria za usalama barabarani, na huwa wanakumbushana mwendo wa familia. Ajali haina kinga, lakini tuna uwezo wa kuzuia isitokee," anasema.

KIINI CHA AJALI

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi Ramadhan Ng’azi, anatoa wito kwa familia wanaposafiri pamoja kuwa waangalifu barabarani.

"Tumezoea kuona wakati wa sikukuu mwishoni mwa mwaka au katika matukio ya kijamii yanayopelekea wanafamilia husafiri chombo kimoja, kwa kuwa wanakuwa wanafahamiana umakini barabarani mara nyingi hupungua.

"Unakuta wanapita hoteli mbalimbali wanapata chakula au vinywaji vinavyowaondolea umakini barabarani hasa safari ndefu wanaona ni sehemu ya kufurahi na kunywa bia.

"Wito wetu ni huu; siku zote watu wanapokuwa safarini iwe wanafamilia au wengine, umakini uongezwe kwa kuzingatia kwamba katika safari za familia kama dereva ni mmoja wawe makini.

"Unakuta mtu hajawahi kusafiri umbali mrefu, mfano Dar-Bukoba au Dar-Mbeya, Dar-Arusha au Dar-Manyara, uchovu unakuwa mwingi.

"Amezoea Kimara-Posta, hivyo kwa umbali mrefu anakuwa hana uzoefu, lakini hapohapo anakunywa vinywaji ambavyo haviruhusiwi au vyakula ambavyo vitamfanya kusinzia," anasema.

Kamanda Ng’azi anasema mara nyingi ajali hizo hutokea kwa sababu za uchovu wa kiakili na kimwili, kula na kunywa vinywaji vinavyoleta usingizi wawapo safarini, kutokuwa na uzoefu wa kuendesha masafa marefu na kutojua barabara vizuri.

"Uzoefu, ulevi na uchovu huchangia kwa kiasi kikubwa ajali za magari binafsi kwa kuzingatia kwamba kwa muda mrefu mtu hajasafiri kwenda kwao, unakuta barabara zimetengenezwa na kuwekewa tahadhari, lakini hajui; mwisho wa siku anatumbukia huko.

"Sababu nyingine ni za kila siku zinazohusu mwendokasi, kupita gari lingine bila kuchukua tahadhari," anafafanua Kamanda Ng'azi.

JAMII YAONYA

Elizabeth Stanslaus, mkazi wa Kimara, wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam, anashauri wanafamilia wanapotaka kusafiri ili kuepuka changamoto mbalimbali ikiwamo ajali, ni vizuri wakasafiri katika vyombo tofauti vya usafiri badala ya kutumia gari moja.

Michael Valentine, mkazi wa Mwenge, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, anasema ndugu wakiamua kutumia gari moja, basi wazingatie kanuni za usalama barabarani na kuchukua dereva mzoefu wa barabara.

"Si kila dereva anaweza kwenda mwendo mrefu, kama umezoea ruti fupi halafu ukaenda safari ndefu huku umebeba familia ni kujihatarisha kwa sababu kuna kuchoka au wakati unaendesha unaanza kukizoea chombo na mwishowe umakini unapungua," anasema.

 AJALI MIAKA 6

Zikirejewa ripoti za matukio ya ajali za barabarani zinazosabisha vifo vya ndugu kwa wakati mmoja katika kipindi cha miaka sita iliyopita, zinajumuisha:

Juni 24, mwaka huu, wanafamilia wanne waliokuwa wakitokea harusini Dar es Salaam walipata ajali eneo la Bwiko, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga. Waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo ni Cecilia Luka (mama mzazi wa bwana harusi), Antonio Luka (dada yake), Judith Michael (42) na Godfrey Michael, waliokuwa katika gari dogo aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 979 CZM. Wote walikuwa wakazi wa Rombo.

Februari 3, mwaka huu, msiba wa aina hiyo ulikumba familia ya ukoo wa Mrema katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, baada ya kupoteza watu 16 kwa ajali ya barabarani.

Walikuwa wanasafirisha mwili wa Athanas Mrema (59) kwa gari. Ajali hiyo ilitokea eneo la Magira Gereza, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, barabara ya Segera/Bwiko, baada ya lori la mizigo aina ya Mitsubishi Fusso lenye namba za usajili T 673 CUC, kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Toyota Coaster, lenye namba T 863 DXN (Special Hire) walimokuwa.

Novemba 28, 2023, bibi harusi mtarajiwa Rehema Chao (37) na mama yake mzazi, Agness Chao (75), walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Raum, kugongana uso kwa uso la lori la mizigo katika eneo la Kisangara, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Ajali hiyo ilitokea baada ya Rehema aliyekuwa akiendesha gari hilo, kukwepa shimo na kugongana na lori. Bibi harusi huyo alikuwa akiendesha gari hilo (Raum) kutoka Morogoro kwenda nyumbani kwao Msae-Marangu ili kuwahi harusi yake iliyokuwa ifungwe siku chache zilizokuwa zinafuata jijini Arusha.

Aprili 25, 2023, majira ya asubuhi, watu wanne wakiwamo watatu wa familia moja, walifariki na wengine wawili kulazwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa na mafuriko katika eneo la King’ori, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, wakati wakielekea kwenye mahafali ya binti yao mkoani Kilimanjaro.

Ndugu waliofariki katika tukio hilo ni Martha Metili (40) na mtoto wake Lissa Metili (8) na Collin Lyimo (16).

Watu hao walikuwa wakitumia gari lao aina ya Toyota Noah, lenye namba za usajili 499 DMY, kusombwa katika barabara ya Arusha/Moshi, eneo la Kata Amarura Tarafa ya King’ori, Wilaya ya Arumeru.

Juni 22, 2023, Mrakibu wa Jeshi la Uhamiaji Kurasini, Dar es Salaam, Martin Mhagama (45) na mkewe Rehema Sekhao (40), walipoteza maisha katika ajali ya gari iliyohusisha basi la abiria, mali ya Kampuni ya Kilimanjaro Express na gari dogo aina ya Toyota Corola.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Majengo, Hedaru, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wakati ofisa huyo na mkewe wakitokea Dar es Salaam kwenda Moshi.

Julai 4, 2023, walifariki dunia watu wanne wa familia moja wilayani Masasi, mkoani Mtwara, baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kugongana na lori aina ya fuso lenye namba za usajili T 522 BBQ.

Agosti 2, mwaka 2023, watu wanne wa familia moja walifariki dunia katika ajali iliyotokea Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Oktoba 11, 2022, Sajini wa Jeshi la Uhamiaji nchini na Ofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Silvester Chambo (36), alifariki dunia kwa ajali ya gari, akiwa na ndugu saba wa familia moja.

Chambo, akiwa anaendesha gari lake aina ya Toyota Corola, lenye namba za usajili T 618 AWP, lililokuwa likitokea Muheza Tanga, liligongana uso kwa uso na Voxywagen lenye namba T 515 DMV, mali ya Honoratus Swai, Mkazi wa Dar es Salaam aliyekuwa akitokea Moshi.

Oktoba 11, 2022, watu watano wakiwamo wawili wa familia moja waliokuwa wakienda msibani Kyela, walifariki dunia katika ajali iliyohusisha basi dogo aina ya Coaster na basi la Kampuni ya Kyela Express baada ya kugongana uso kwa uso eneo la Kiwira, wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.

Novemba 26, 2022, Immaculate Byemerwa (49) pamoja na watoto wake wawili, Jolister Byemerwa (17), mhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Gili ya Kibaha na Janeth Byemerwa (20), mwanafunzi aliyekuwa anasoma mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walipoteza maisha wakitoka katika sherehe ya mahafali Kibaha mkoani Pwani.

Chanzo kikiwa ni gari aina ya Prado Land Cruiser walilokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kuacha njia na kuangukia katika bonde. Katika ajali hii kulikuwa na majeruhi mmoja.

Mwezi Aprili, 2018, watu wanane wa familia moja walifariki dunia papo hapo na mmoja kujehuriwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka wilayani Chunya kwenda mjini Mbeya, kugongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Igembesabo katika eneo la Igodima barabara kuu ya Mbeya- Tabora nje kidogo ya Jiji la Mbeya.

Mei 29, 2018, mkoani Rukwa, watu watatu wa familia moja walifariki dunia katika ajali iliyohusisha pikipiki iliyokuwa imebeba wanafamilia hao na basi mali ya Kampuni ya Saratoga.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati anawasilisha bungeni Juni 13 mwaka huu mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25, alisema ajali za barabarani zinagharimu maisha ya watu wengi nchini, akishauri kufanywe mabadiliko ya sheria ili wanaosababisha ajali washtakiwe kwa jinai ya mauaji. 

Dk. Mwigulu alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2019 hadi Mei 2024), ajali za barabarani nchini zilikuwa 10,093 zikisababisha vifo vya watu 7,639 na kujeruhi watu 12,663, wakiwamo waliopata ulemavu wa kudumu.

"Hebu fikiria, magari binafsi - ajali 3,250, vifo 2,090, majeruhi 3,177. Hebu fikiria, mabasi - ajali 790, vifo 782, majeruhi 2,508. Hebu fikiria, daladala - ajali 820, vifo 777, majeruhi 1,810. Hebu fikiria, taxi - ajali 93, vifo 97, majeruhi 173. Hebu fikiria, magari ya kukodi (sherehe, misiba, na shughuli maalum) - ajali 326, vifo 263, majeruhi 302. 

"Idadi hii kubwa ya majeruhi na vifo vya watu kutokana na ajali utadhani nchi iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe," alitamka Waziri Mwigulu kwa hisia kali bungeni.