RC Mwanza awaomba wafanyabiashara wafungue maduka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:48 PM Jun 27 2024
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoa huo lengo likiwa ni kuwasikiliza michango na maoni yao juu ya mgomo huo unaoendelea Jijini Mwanza.

Katika mazungumzo yake Mkuu Mkoa amewasihi wafanyabiashara wote waliofunga maduka yao kuhakikisha wanayafungua kwa hiari yao wenyewe kwani Serikali ya Mkoa wa Mwanza ipo tayari kusikiliza hoja zao.
 
Akiongea mara baada ya kuwasikiliza wafanyabiashara hao wanaolalamikia utitiri wa kodi kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mtanda amesema hakuna Taifa linaloweza kujiendesha bila kodi hivyo Serikali inakuwa na uwezo wa kuwahudumia na kupeleka miradi kwa Wananchi kutokana na michango inayotolewa na Wananchi wenyewe ikiwemo ulipaji wa kodi lakini amesema changamoto ambazo zimetajwa kuwakera wakati wa ukusanyaji kodi zitashughulikiwa.
 
RC Mtanda amesema endapo Wafanyabiashara hao wanataka sheria za kodi zibadilishwe basi hawana budi kupeleka maoni yao ili Wabunge wayachukue na wakayafanyie kazi Bungeni maana chombo pekee kinachoweza kuunda na kuvunja sheria ni Bunge na si vinginevyo.