Prof. Janabi: Wananchi wa Arusha wana presha kubwa ni hatari

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 05:57 PM Jun 27 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi, amesema wananchi wa mkoa wa Arusha wanaongoza kuwa na Shinikizo la damu kwa kiwango kikubwa cha 180 kwa 110 kutokana na matumizi ya chumvi nyingi katika ulaji wa nyama.

Profesa Janabi aliyasema hayo leo wakati akitoa elimu kwa wananchi waliojitokeza katika kambi maalum ya siku saba ya utoaji wa huduma bure kwa wananchi jijini Arusha.

“Hisia yangu kubwa wanatumia chumvi nyingi kwenye nyama. Presha za Arusha zinatia wasiwasi kama tusipochukua hatua za makusudi matatizo ya magonjwa ya moyo, kiharusi na figo yatakuwa ni makubwa katika huu mkoa,”amesema.

Amesema kwa wagonjwa aliowahudumia leo wamebainika kuwa na kiwango kikubwa cha shinikizo la damu jambo ambalo linahatarisha afya zao kwa kuwa wanaweza kupata magonjwa.

“Wagonjwa wengi wamekutwa na shinikizo la juu la damu ni muhimu muelewe duniani kwa sasa kuna karibu bilioni 1.2 wana matatizo ya presha na asilimia 32 ya vifo vyote vinavyotokea duniani ni kwa ajili ya magonjwa ya moyo ambayo yanawekwa katika magonjwa yasiyoambukizwa,” amesema.

Janabi amesema changamoto kubwa ya shinikizo la damu ni kwamba haina dalili “Nimemsikia mgonjwa mmoja anasema yeye akiwa na presha kichwa kinamuuma naomba nilisemee hivi ukiwa na ugonjwa wa homa ya matumbo (Typhoid) kichwa kitauma, ukiwa na UTI kichwa kitauma na ukiwa na njaa kichwa kinauma maana yake sio dalili ya ugonjwa mmoja wa presha,”

Amesema namba za ugonjwa wa kiharusi zinapanda kwa kasi kutokana na watu wengi wana tatizo la shinikizo la damu wanatembea nao bila wao kujua.