Wazazi warahisishiwa mchakato ulipaji ada mashuleni

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:54 PM Jun 27 2024
Wazazi warahisishiwa mchakato ulipaji ada mashuleni.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wazazi warahisishiwa mchakato ulipaji ada mashuleni.

KATIKA kuunga mkono jitihada za serikali kwenye utekelezaji wa dira ya kukuza uchumi wa kidigitali pamoja na kuhakikisha mifumo mbalimbali muhimu inasomana, Airtel Tanzania imezindua mfumo maalumu utakaowarahisishia wazazi mchakato wa kufanya malipo ya ada shuleni kwa usalama.

Kampuni hiyo ya mawasiliano imeeleza kuwa mfumo huo umetengenezwa mahususi kwaajili ya kuhakikisha usalama wa fedha pamoja na kuepusha changamoto za udanganyifu au utapeli ambao wazazi wanaweza kukutana nao wakati wa kufanya malipo kwaajili ya ada kwa watoto wao.
 
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam Mkuu wa kitengo cha Malipo Airtel Money, Janeth Kwilasa, amesema mfumo huo utamuwezesha mzazi kuona kiasi halisi cha ada anachotakiwa kulipa, hali itakayookoa muda ambao angeupoteza kuwasiliana na shule husika ili kupewa taarifa hizo.
 
“Mfumo huu sio kwa malipo tuu uko kwa uzito wake tulizingatia vitu vingi na kuangalia kitu gani ni maumivu kwa shule na taasisi za namna hiyo tukagundua kwamba pia kuna uhitaji wa kuwa na ripoti ambazo zinamjumuisho wa taarifa zote zinatokea shule ambazo ni muhimu mzazi kuzifahamu.
 
“Ikiwemo mchanganuo wa matumizi ya fedha wanazolipa, kuwasiliana na wazazi katika shughuli mbalimbali pamoja na kuwa na uangalizi mzuri wa kalenda ya mwaka. Na mfumo huu utatolewa katika shule zote bila gharama yoyote, nia yetu ni kusaidia wazazi na shule kumudu kazi zake kwa ufanisi na usalama,” amesema Janeth.
 
Ameongeza kuwa, ili mzazi kupata taarifa zote muhimu zinazomhusu mwanae baada ya kuingia kwenye mfumo atatakiwa kuweka kumbukumbu namba ya mtoto wate, kwakuwa programu hiyo itakuwa na uwezo wa kuvuta taarifa za motto kutoka kwenye shule aliko.
 
Aidha, ameeleza kuwa hata wakati wa kufanya malipo ataambiwa anamlipia mtoto Fulani, katika shule ipi na anasoma darasa gani na itamuwezesha kufanya uhakiki, akieleza kwamba mfumo hupo pia utachoche aukuaji wa uchumi pamoja na utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya karatasi.
 
Mwalimu mkuu wa shule ya ‘Fountain Gate’ Fredi Chalewa, aliewawakilisha wakuu wa shule zingine zinazotumia mfumo huo, amesema hatua hiyo imeigusa sana jamii kwasababu mfumo umejibu changamoto ambazo wamekuwa wakizipitia kwa muda mrefu.
 
“Wakati tunafikiria namna gani tutajibu changamoto ambazo zilikuwa zinatukabili hasa pale ambako wazazi wanalipa, ada benki anaondoka na ‘pay sleep’ anakuja tena shuleni, tuthibitishe, tupige tena simu benki tuhakikishe,  alafu tumrudie tena kuthibitisha kuwa amelipa, mlolongo ulikuwa ni mrefu sana.
 
“Ukizingatia wakati mwingine wazazi wako kazini au kwenye biashara zao kwakweli ilikuwa ni ngumu sana, tunashukuru Airtel Tanzania kwa hatua hii tutakuwa tumepumzika hata wazazi wengi tulipowashirikisha wamefurahi juu ya hili,” amesema Chalewa.