BENKI ya Biashara ya Mwalimu (MCB) imesema itaendelea kuzingatia miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania katika kulinda amana za wateja na kuchukua hatua thabiti kuhakikisha wanaboresha usalama wa fedha kidijitali ili kupambana na uhalifu wa kifedha kwa njia ya mtandao.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa nane wa Wanahisa uliofanyika leo Mkoani Iringa, Afisa Mtendaji Mkuu wa MCB, Richard Makungwa, alielezea kuwa benki hiyo katika uendeshaji wa kidijitali, akibainisha kuwa takriban asilimia 95 ya miamala ya benki sasa inafanyika kidijitali.
Makungwa aliwahakikishia wadau wa benki hiyo kuwa mifumo ya hali ya juu ya kuzuia udanganyifu na usalama wa mtandao ya MCB inasimamiwa na idara maalum ili kulinda fedha za wateja muda wote.
Katika hotuba mgeni rasmi iliyosomwa na Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, aliyepaswa kumwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) alisema serikali itahakikisha inakuwa na ushirikiano thabiti na taasisi za fedha ikiwemo benki hiyo.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa serikali unalenga kutatua changamoto ndogo ndogo zinazokabili benki hiyo na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
"Serikali itaendelea kushirikiana na benki hii na taasisi nyingine za fedha katika kutatua changamoto zilizopo ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kirahisi," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED