TLS kuanza mchakato uandikishaji rasimu Katiba Mpya

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:01 PM Jun 27 2024
Rais wa TLS, Wakili Mwandamizi Harold Sungusia.
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais wa TLS, Wakili Mwandamizi Harold Sungusia.

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimekusudia kuanza mchakato wa kuandika rasimu ya Katiba Mpya ambayo itasimamiwa na chama hicho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kupata Katiba itokanayo na maoni ya wananchi.

Aidha, TLS imekusudia kuteua kamati maalum ya wataalam wa Katiba watakao kaa na kuandika sheria ya mabadiliko ya Katiba pamoja na Rasimu.

Wabobezi wa Katiba kutoka taasisi mbalimbali wakiwamo wahadhiri  kutoka vyuo vikuu, maprofesa na wanaharakati wamekutana katika Ofisi cha Chama cha Wanasheria Tanganyika ( TLS) kujadili mchakato  wa kupata Katiba mpya.

Kikao hicho kilikuwa na lengo  la kuangazia Mkwamo wa kupata Katiba Mpya uliotokea mwaka 2014. Mjadala huo uligusia juu ya “Ni wapi tulipokosea na kusababisha mkwamo, tunarekebishaje ili tusikwame tena, tunaanzia wapi ili kutoka kwenye mkwamo na mambo ya muhimu kuyazingatia katika mchakato huo”.

Akifungua mjadala huo jana, Rais wa TLS, Wakili Mwandamizi Harold Sungusia, amesema ni muda muafaka kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya ambayo itabeba majibu ya wananchi kuhusu mambo wanayoyataka kwa ustawi wao.

1

Amesema Chama hicho kinabariki kuendelea na mchakato wa kupata kamati ya wataalam watakao tukika kuandaa sheria na Rasimu ya Katiba Mpya ambapo kabla ya tar 05 Julai kamati ya TLS inayoshughulikia Maboresho ya Katiba itapaswa kuwa imependekeza timu hiyo ya wataalam

Akichangia mada katika kikao hicho, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Tanzania, Robert Makaramba amesema ili kupatikana kwa Katiba mpya TLS isimamie mchakato huo kikamilifu bila kuingiliwa na watu wengine kwa ajili ya kuleta matokeo chanya.

“TLS ndio mbebe hii dhamana ya kupatikana kwa Katiba mpya ambayo itatufaa wananchi; mfanye jambo litakaloonekana kuwa na manufaa kwa watanzania wote;  hakuna mmiliki wa Katiba iliyopo wala itakayokuja, kila mtu anapaswa kutoa maoni na mapendekezo yake,” amesema Jaji Makaramba.
2

Dk. Ananilea Nkya, ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) amesema miongoni mwa mambo watakayoyafanya ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za kiuchumi zitokanazo na Katiba iliyopo sasa.

Amesema fedha nyingi zinatumika katika kuendesha Bunge, Serikali na masuala mengine ambayo ingekuwepo Katiba mpya yasingekuwepo. Aidha, alisema baada ya kukamilika kwa kamati ya TLS watazunguka mikoa yote nchini kutoa elimu juu ya umuhimu wa Katiba huku wakiihusisha na maisha ya wananchi.

Thobias Messanga, kutoka Jukwaa la Katiba na Tanzania, (JUKATA), amesema michakato iliyotanguliwa kuhusu Katiba mpya haijafanikiwa kwa sababu ya baadhi ya watu kuingiza maslahi yao  binafsi.

Amesema baadhi ya wafanya maamuzi wanashindwa kusimamia upatikanaji wa Katiba mpya kwa sababu za kisiasa na kufanya  kama mradi wa  kujipatia pesa.
3

“Wapo baadhi ya watu ambao hawatakubali kutengeneza Katiba mpya ambayo itaendana na matakwa ya wananchi, ushiriki wa Katiba mpya kwa asilimia kubwa uliegamia upande mmoja wa chama cha kisiasa, tuondoke huko, sisi kama wanasheria tunalo jukumu la kuhakikisha tunalisaidia taifa letu kupata Katiba ya wananchi na sio iliyopo,” amesema Messanga.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Dk. Thobias Mnyasinga alisema uwakilishi juu ya rasimu zilizopita haukuwa sahihi, lakini muda wa kusahihisha makosa upo na kwa sasa wananchi wanapaswa kuelewa na kueleza wanachokitaka kwenye Katiba mpya.

Prof. Azaveli Lwaitama, ambaye ni mhadhiri mstaafu amesehauri TLS wasiitegemee serikali kuendesha mchakato huo badala yake watengeneze muswada wao ambao  utakuwa na uchambuzi wa kutosha   na utajumuisha masuala yote ili kupata Katiba mpya iliyo bora.