Marekani yamfunga miaka 45 jela Rais wa zamani wa Honduras

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:10 PM Jun 27 2024
Rais wa zamani wa Honduras, Juan Orlando Hernandez .
Picha: Maktaba
Rais wa zamani wa Honduras, Juan Orlando Hernandez .

MAHAKAMA ya Mji wa New York nchini Marekani, imemhukumu Rais wa zamani wa Honduras, Juan Orlando Hernandez (55) kifungo cha miaka 45 jela na faini ya dola milioni nane kwa makosa ya ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Hernandez amehukumiwa kwa kuyasaidia makundi ya wauzaji wa dawa za kulevya tani 500 za cocaine kuingiza nchini Marekani. Waendesha mashitaka wa Marekani wamesema Hernandez aliigeuza Honduras kuwa taifa la dawa za kulevya wakati alipokuwa rais kuanzia mwaka wa 2014 hadi 2022.

Wamesema alitumia fedha hizo kujitajirisha na kufanya udanganyifu katika uchaguzi nchini Honduras. Jaji Kevin Castel alimuelezea rais huyo wa zamani kuwa ni mwanasiasa mwenye nyuso mbili ambaye alikuwa na uchu wa madaraka. 

DW imeripoti kuwa, Hernandez ameiambia mahakama kuwa hakuwa na hatia na alikuwa ameshitakiwa bila haki. Rais huyo wa zamani wa Honduras awali alidokeza kupitia mawakili wake kuwa angekata rufaa kupinga hukumu hiyo.