Serikali: Nyongeza ya asilimia 7 kikokotoo si haba, isibezwe

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:27 AM Jun 27 2024
Naibu Waziri wa Fedha, Ahmad Chande.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri wa Fedha, Ahmad Chande.

NAIBU Waziri wa Fedha, Ahmad Chande, amesema nyongeza ya asilimia saba kwenye kikokotoo cha mafao ya wastaafu ni kitu kikubwa kisichopaswa kubezwa.

Chande ameyasema hayo bungeni wakati akichangia mjadala wa mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

"Kutoka asilimia 33 hadi 40 ni kikubwa sana na Mheshimiwa Spika, hata kama ingekuwa asilimia moja tu ingekuwa ni hatua kubwa sana kwa sababu wahenga wanasema 'jicho hutaraji haja kila namna na penye moja na moja si moja tena'. Kwa hiyo, hata ingekuwa moja ingetosha," amesema.

Chande amesema wafanyakazi wengi wameshukuru na baadhi ya wabunge wametoa shukrani kuhusu jambo hilo, akisisitiza "asiyeshukuru kwa yai, basi na jogoo hachinjiwi".

Naibu Waziri huyo pia amesema watafanyia kazi ushauri ulitolewa na Kamati ya Bajeti kuhusu mikopo ambayo inakopwa na serikali ielekezwe kwenye miradi ya uzalishaji.