Mgomo wa wafanyabiashara wasambaa kusini, nyanda za juu

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:59 AM Jun 27 2024
Mgomo wa wafanyabiashara.
Picha: maktaba
Mgomo wa wafanyabiashara.

BAADHI ya wafanyabiashara wenye maduka katika mikoa minne wameungana na wenzao wa Soko la Kimataifa Kariakoo kufunga biashara zao, huku mkoani Arusha wakitumia muda huo kucheza mpira wa miguu.

Mikoa mingine ambayo baadhi ya wafanyabiashara wake walifunga maduka jana ni Njombe, Mtwara na Songwe, huku baadhi  ya wafanyabiashara katika Soko la Kimataifa Kariakoo pamoja na wa mikoa ya Mbeya na Mwanza wakiendelea na mgomo huo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amekutana na viongozi wa wafanyabiashara katika kikao cha ndani jijini Dodoma, kikitanguliwa na kile kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii kikihusisha viongozi wao na serikali.

Jumatatu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alitoa maazimio, ikiwamo kusitisha ukaguzi wa risiti za Kielekroniki (EFD) na ritani za kodi uliokuwa unafanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Mkoa wa Kikodi Kariakoo.

WACHEZA MPIRA

Jijini Arusha, wafanyabiashara wamefunga maduka yao kwa zaidi ya saa sita na kutumia muda huo kucheza mpira na baadaye baadhi yao walifungua.

Christopher Jengele, mmoja wa wafanyabiashara hao amesema kuwa badala ya kushika mawe kuanza kupiga watu na kuwaumiza, wameona ni bora kucheza mpira ili kujenga afya wakisubiri viongozi wao kutoa kauli ya ama kufungua maduka au kuendelea na mgomo.

Amesema wamefunga maduka kwa kuwa wanaumia; wanalipa kodi ya chumba cha biashara Sh. milioni tatu kwa mwezi, ilhali machinga wanauza mbele ya maduka yao na hawatozwi kodi yoyote.

Frank Laizer, mfanyabiashara mwingine jijini, amesema wamefunga maduka yao kuunga mkono wenzao waliotangulia kufanya hivyo kutokana na utiriri wa kodi unaowaumiza.  

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Kirenga Sway, amesema hawatambui mgomo huo na kuagiza wafanyabiashara wafungue maduka yao.

Katibu wa Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Ahmednoor Jamal, amesema wafanyabiashara wasubiri tamko kutoka kwa viongozi wao wa kitaifa ili kujua serikali imekubali mambo mangapi kati ya hoja 28 walizowasilisha.

Mnunuzi wa bidhaa, Eliah Mteshibe, amesema serikali na wafanyabiashara hao wanapaswa kumaliza changamoto zao ili kutoa fursa kwao kununua bidhaa na kupeleka vijijini kuuza.

Wakati hali ikiwa hivyo jijini Arusha, wafanyabiashara katika Soko Kuu la Mtwara wametaja sababu ya kufunga maduka kuwa ni kutokana na viwango vya kodi walivyokuwa wakilipa awali kuongezeka katika mabanda yao ya biashara.

Issa Bakari, mfanyabiashara mkoani Mtwara, amesema kumekuwa na ongezeko la kodi katika mabanda, linalotishia uhai wa biashara zao.

Mkoani Mbeya, mgomo huo umeingia siku ya tatu. Masoko ya Mwanjelwa, Sido, Kabwe na Sokoine kulishuhudiwa shughuli kusimama na kuonekana watu wachache wakiwamo walinzi.

Mama lishe, Asha Mwakibinga, anayefanya shughuli zake katika soko la Mwanjelwa, amesema amepunguza kipimo cha chakula kutokana na uhaba wa wateja.

Mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana, amesema walizungumza na wafanyabiashara jana asubuhi kuwaeleza walichoteta na serikali na kuendelea kuwaomba wafungue maduka yao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema kuwa wafanyabiashara watakaoona inafaa kufungua biashara zao wakati serikali ikiendelea kushughulikia changamoto zilizojitokeza, wafanye hivyo na wanaoona haifai waendelee kugoma.

"Tumewaita (wafanyabiashara) mmekataa  kuja, sasa tutapataje suluhisho? Mnatakiwa kujenga utamaduni wa kukutana na kufanya mazungumzo pindi kunapotokea kutokuelewana. 

"Mimi na menejimeti ya mkoa tupo,TRA, TANESCO, Mkurugenzi wa Jiji na wataalamu wanaohusika kukusanya kodi wapo hapa, tungejadiliana, lakini walalamikaji hawapo, tunawasaidiaje?" Mtanda amehoji. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania wa Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati, amesema hakuna kiongozi yeyote wa jumuiya hiyo aliyehudhuria kikao hicho kwa kuwa barua ya wito wa kikao hicho walipata usiku.

Mfanyabiashara Soko la Makambako mkoani Njombe, Atukuzwe Ilomo,  amesema licha ya serikali mwaka uliopita kukusanya maoni yao, kero bado ni nyingi, ikiwamo utozwaji Sh. milioni 15 wanapokutwa hawajatoa risiti.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani humo, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Siphael Msigala, amesema serikali inapaswa kuweka kodi katika makundi mawili ili kuondoa mrundikano kwao.

FREEMAN MBOWE

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akizungumza na wananchi wa Kata ya Dongobesh, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara amesema hawapaswi kumtoza kodi mtu ambaye hawajui kipato chake.

Amesema Watanzania wengi wanafanya kazi ngumu na kipato chao hakifanani na gharama za maisha.

"Mmesikia leo, tangu juzi wafanyabiashara wamegoma Dar es Salaam, si mmesikia? Wafanyabiashara wakubwa wanaosambaza bidhaa mbalimbali nchi nzima na wanaoagiza nje wamegoma.

"Wamegoma, wanasema 'biashara imekuwa kero, tunateswa na maofisa wa TRA, mitaji yetu inafilisika kwa ajili ya kodi. Tukigeuka kodi, tukigeuka faini'. Mtu anakuambia ana biashara ya mtaji wa milioni tano, anapigwa faini milioni 15.

"Wafanyabiashara wamesema, 'kuliko tuendelee kufanya biashara, bora tufunge maduka'. Kariakoo kwa taarifa yenu, katika 'maokoto' ya kodi, hiyo biashara ya Kariakoo inachangia zaidi ya asilimia 60 ya mapato ya taifa, wamefunga maduka," amesema Mbowe.

Katika Mji wa Tunduma, mkoani Songwe zaidi ya maduka 500 katika Soko la Manzese na Soko Kuu la Halmashauri ya Mji wa Tunduma jana hayakufunguliwa.