Mbowe: Miaka 7 kila kona malalamiko

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:39 AM Jun 27 2024
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Picha: Maktaba
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Tanzania ni nchi pekee isiyo na vita, lakini wananchi wake wakati wote wanalalamika.

Amesema miaka saba iliyopita ni miongoni mwa nchi za mwisho tano zisizo na furaha.

Jana, akiwa Kata ya Dongobesh, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara katika mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Mbowe amesema wanajiuliza nchi haina vita, lakini hizo nchi nyingine ambazo hazina furaha, zina vita.

“Tujadili maisha yetu, tumetoka wapi, tuko wapi na tunapaswa kwenda wapi. Ni jambo la bahati mbaya sana, karibu kila mahali wanalalamika, kila unapokwenda watumishi wanalalamika, kila unapokwenda wanafunzi wanalalamika.

“Kila unapokwenda nchi hii wafugaji wanalalamika. Kila mahali kuna kilio, wanalalamika. Tunajiuliza kwa nini Watanzania hawana furaha. Umoja wa Mataifa wanafanya survey ambayo inaitwa World Happiness Index, yaani unapima mataifa na raha ya kila taifa.

Tanzania ndio nchi pekee isiyo na vita, lakini wananchi wake wakati wote wanalalamika. Wananchi wanalalamika kwa sababu mbalimbali.”

Mbunge wa zamani wa Arusha na Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema:

"Leo tunafanya mikutano mitano. Nilikuwa natafuta hizi data (takwimu), Tanzania wananunua maziwa kila mwaka bilioni 34.5 kutoka nje ya nchi.

"Nyie mkipewa ng’ombe zinazozalisha maziwa kwa wingi, mkatengenezewa mashamba ya kuzalisha vyakula vya ng’ombe, hamuwezi kufuga ng’ombe nyie?"

"Mahindi pamoja na kulima wanaleta ya bilioni 64, sukari bilioni 265, mchele tunanunua kila mwaka bilioni 146, maharage ya soya bilioni 34, njano bilioni 554 na mafuta ya kula bilioni 694. Jumla yake karibu trilioni mbili.

Vyakula vyote hivi, bidhaa zote hizi zinaweza kulimwa Mkoa wa Manyara peke yake. Yaani maana yake trilioni mbili ikibaki Manyara kila mwaka kwenye mazao huku tusingeona lami za kubabaisha, kungekuwa na lami, kungekuwa na vyuo, watoto wangesoma na watu wangekuwa na maisha bora. 

Uchumi ni maarifa, ndio sababu Abu Dhabi (Makao Makuu ya Falme za Kiarabu-UAE), ni jangwa, lakini wana uchumi mzuri kuliko Tanzania.

"Hanang’ kuna shamba la ngano, yale mashamba yamekufa. Leo tunaagiza ngano ya bilioni 500 Ukraine. Jiulize bilioni 500 ingekuwa inabaki Hanang’ kila mwaka Hanang’ ingekuwa kubwa kuliko Dar es Salaam. Kahawa, Mwenyekiti (Mbowe) anajua zaidi kuhusu kahawa.

Kahawa imesomesha vijana wote wa Kichaga. Kahawa imesomesha vijana wote wa Kagera, kahawa ni zao la pili duniani baada ya mafuta kwa kuuzika.

"Kahawa leo imekufa Kilimanjaro, kahawa imekufa Kagera, kahawa imekufa kila mahali. Hata yale mazao yanayoota bila mbolea nchi hii imeshindwa kuyasimamia."