Serikali inakiongezea uwezo Kituo cha kupoza umeme Mbagala- Kapinga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:27 PM Jun 27 2024
Naibu Waziri wa Nishati,Judith Kapinga.

Naibu Waziri wa Nishati,Judith Kapinga amesema Serikali inafanya upanuzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mbagala mkoani Dar es Salaam ili kukiongezea uwezo utakaoondoa changamoto ya kukatika kwa umeme katika eneo hilo la Mbagala.

Kapinga amesema hayo leo Juni 27, 2024 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbagala,Abdallah Chaurembo aliyetaka  kufahamu Serikali itakomesha lini changamoto ya kukatika kwa umeme katika Jimbo la Mbagala.

Mbali na upanuzi wa kituo hicho cha Mbagala ambacho kinaongezewa transfoma ya 120MVA,Kapinga amesema kwa hivi sasa hali ya upatikanaji umeme imeimarika Mbagala tofauti na ilivyokuwa mwaka jana.

Aidha, wakati  akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo Vijijini,Muharami Mkenge aliyetaka kufahamu lini mradi wa kupeleka umeme katika eneo la Kitume Kata ya Makurunge - Bagamoyo utaanza,Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi ya kupeleka umeme katika maeneo ya Bagamoyo.

Ameongeza kuwa, katika Kata ya Makurunge eneo la Kitume, REA inatekeleza mradi uitwao Electrification of Small Scale Mining, Industries and Agricultural Ares in Mainland Tanzania kupitia mkandarasi M/s Dieynem Company Limited.

Amesema  mradi huo ulioanza mwezi Machi 2023, umefikia asilimia 57 ambapo kwa sasa mkandarasi amekwishasimika nguzo kwa umbali wa kilometa 9. 

Akizungumzia changamoto ya kuchelewa kukamilika  kwa mradi huo, Kapinga amesema kulitokana na maji ya mvua kujaa katika eneo kubwa ambalo mkandarasi anafanyia kazi na kuongeza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwezi Desemba, 2024.

Kuhusu wananchi wa Kitongoji cha Sangwahela kilichopo katika kata ya Mapinga kupata huduma ya umeme, Kapinga amesema Serikali imepokea suala hilo na itafanyia tathmini ili kuweza kuwafikishia umeme wananchi wa maeneo hayo.