NEMC yaonya wacheleweshaji wa malipo ya tozo za mazingira

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 12:53 PM Jun 27 2024
Msimamizi wa Tozo na Ada mbalimbali wa baraza la NEMC, Canisius Karamaga.
Picha: Maktaba
Msimamizi wa Tozo na Ada mbalimbali wa baraza la NEMC, Canisius Karamaga.

BARAZA la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeelekeza wawekezaji wa miradi mbalimbali kulipa tozo na ada za mazingira wanazodaiwa kabla ya kupigwa faini kwa kushindwa kuzilipa kwa wakati.

Msimamizi wa Tozo na Ada mbalimbali wa baraza hilo, Canisius Karamaga, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema ada hizo ni muhimu kwa ajili ya kuliwezesha baraza kutekeleza shughuli zake za msingi lilizopewa kisheria na kuwawezesha wananchi kuwa salama kwa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya miradi kuanza.

"Tozo hizi ndizo zinasaidia NEMC kutekeleza majukumu yake kwa wakati. Kwa mfano, tunapopata taarifa ya mafuriko au kimbunga, maofisa wetu wanakwenda kuangalia maeneo husika na kufanya tathmini ya kina," amesema.

Karamaga amesema kuwa baada ya tathmini hiyo, huishauri serikali hatua za kuchukua kuepusha maafa na kazi hizo zote zinafanywa kutokana na ada na tozo hizo.

"Lengo la ada na tozo hizo ni baraza lipate fedha ili miradi ikaguliwe, ipate miongozo iliyo sawa na kufanyiwa tathmini ya athari za mazingira na wawekezaji waweze kushauriwa namna ya kuweza kuendesha shughuli zao bila kuathiri mazingira,” amesema.

Amesema ada na tozo hizo zina utaratibu na muda wa kulipa kwa mujibu wa sheria na kwamba kinyume cha hapo, wale wanaolimbikiza hukumbana na adhabu ya riba ya asilimia tano kwa kila mwezi kwa mhusika aliyechelewesha malipo hayo.

Amesema tozo husaidia baraza kupata fedha kutoka kwa wanaofanya miradi kuwezesha kukaguliwa na kupata vyeti vya tathmini ya athari kwa mazingira.

"Kwa mfano, mwekezaji akitaka kujenga kiwanda, lazima tumshauri namna gani ya kukijenga na namna ya kufanya tathmini ya athari kwa mazingira, vitu gani afanye na vitu gani asifanye. Sasa yote hayo ni gharama, lazima kuwe na fedha," amesema.

Karamaga amesema nia ya kufanya tathmini ya athari kwa mazingira ni kumwezesha mwekezaji kujenga mradi ambao hautasababisha mgogoro na wananchi wanaoishi jirani na kusababisha madhara.

Pia amesema tozo hulipwa kwa njia mbalimbali na katika kanda 12 za NEMC zilizoko nchini ambapo wahusika wamekuwa wakipewa namba za malipo.

Amesema wananchi wamehamasika kulipa ada na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Baadhi wanalipa baada ya kukumbushwa mara kwa mara.

"Wasiolipa kwa wakati tunawaandikia barua, tunawapigia simu, tunawakumbusha kwa njia mbalimbali na wengi huwa wasikivu sana kwa kuwa tukiwakumbusha wanalipa kwa wakati," amesema.

Ofisa huyo pia amesemakuna umuhimu kwa Watanzania kujali na kutunza mazingira kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yanasababisha athari kubwa kwa miundombinu ya nchi na wakati mwingine watu kufariki dunia kutokana na majanga.

"Lazima tuyajali mazingira kwa sababu tukiyapuuza huwa yanatukumbusha umuhimu wake, na ndiyo sababu utaona majanga mbalimbali kama mafuriko, moto, kimbunga na mengine yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi," amesema.