Nyambaya aula tena DRFA, Nyamlani akemea migogoro

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:10 AM Aug 30 2024
LAMECK Nyambaya
Picha: Mtandao
LAMECK Nyambaya

LAMECK Nyambaya amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kwa kupata kura zote 11 katika uchaguzi uliofanyika kwenye Ukumbi wa King Jada jijini jana.

Mkutano huo wa uchaguzi pia ulimuidhinisha Benny Kisaka kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho huku Juma Pinto akichaguliwa kwa kura zote kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kondo Mussa aliyepata kura 10 na Ramadhani Shauritanga (kura sita), walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya DRFA wakati Chichi Mwidege alitangazwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa kuteuliwa.

Mjumbe mwingine wa Kamati ya Utendaji aliyetangazwa jana ni Somoe Ng'itu ambaye anaingia moja kwa moja kwa sababu ni Mwenyekiti cha Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (DWFA).

Akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kujiepusha na migogoro na badala yake kuwekeza nguvu katika kuhakikisha soka linachezwa kwa ubora wa juu hapa jijini.

Nyamlani alisema Dar es Salaam ndio kioo cha soka hapa Tanzania, hivyo anataka kuona ushindani wa ligi zake unarejea kama ilivyokuwa miaka ya nyuma pamoja na kuzalisha waamuzi, makocha na wachezaji mbalimbali.

"Kioo cha mazingira ya mpira wetu ni Dar es Salaam, kuna mahala fulani tulipotea, Dar kukawa hakuna tena ile hadhi yetu hadi ikaondolewa kutoka Kanda na kuwa mkoa kama Katavi au Lindi, hii hapana, tufanye mabadiliko, turudi kule tulipokuwa," Nyamlani alisema.

Aliongeza anataka kuona vyama vya wilaya za Dar es Salaam vinakuwa imara na si sehemu ya 'magenge' ya watu kujitafutia maslahi binafsi.

"Hatutaki migogoro, tunataka katiba mpya, katiba imara, wacheni tuifufue Dar es Salaam, tuweke maslahi binafsi pembeni, matendo yafanane na mkoa wa Dar es Salaam, tutengeneze waamuzi, tuhakikishe waamuzi bora watoke hapa, wenzetu wanampango ndio maana wamefanikiwa kuzalisha waamuzi bora, tuzalishe makocha, tuwe kitovu cha kila kitu cha mpira wa Tanzania," Nyamlani aliongeza.

Baada ya kutangazwa mshindi, Nyambaya aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu na kuahidi kuinyanyua upya Dar es Salaam ili iwe tishio kama ilivyokuwa miaka iliyopita.