Mwimbaji maarufu wa muziki wa taarabu nchini, Ally Hemed maarufu 'Ally Star' amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), atazikwa kesho Februari 04 nyumbani kwao Kilosa mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Bendi ya TOT, Khadija Kopa, amesema taratibu za mazishi zitaanza kesho majira ya saa 2:00 asubuhi kutoka MNH.
Kopa amesema waombolezaji wanatakiwa kukusanyika hospitalini hapo kuanzia saa 1:00 asubuhi tayari kwa safari ya kuelekea Kilosa mkoani Morogoro.
Katika maisha yake ya usanii, Ally Star alitamba na nyimbo za mahadhi ya pwani kama Zumbukuku, Natanga na Njia, hauvumi lakimu humo ambazo zilimpa heshima kubwa katika muziki wa taarab.
Katika uhai wake Ally Star aliwahi kufanya kazi katika bendi za Double Q, Bima Modern Taarabu, na Kikundi cha Muungano (Muungano Cultural Troupe).
Baadhi ya mashabiki, wasanii na wadau wa sanaa wameendelea kuomboleza kifo cha gwiji huyo wamimwelezea kuwa alikuwa ni msanii aliyetoa mchango mkubwa katika kukuza muziki wa taarab.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED