Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga, ameishauri serikali kupunguza utitiri wa mifuko ya kuwezesha vijana, ambayo hivi sasa inaratibiwa na wizara mbalimbali.
Amesema lengo la kupunguza mifuko hiyo ni kuongeza ufanisi na kupunguza malalamiko kwa walengwa kutofikiwa na uwezeshwaji huo.
Sanga amesema hayo leo Februari 03 bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia mjadala kuhusu Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/27-2050/51, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/27-2030/31 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27.
Sanga amesema: “Ripoti zinaonesha kuwa kuna mifuko 70 ambayo inahusika na uwezeshaji vijana lakini ripoti inaonyesha kuwa tumekopesha zaidi ya Sh. trioni 3.5 kwa vijana zaidi ya milioni 24, hasa kama tumekoposha hizi fedha vijana wengi wanalalamika ajira hakuna, nani anayekula hizo fedha?.
“Kwahiyo ni lazima kuwe na kapu moja ambalo litasimamia mifuko yote ambayo inawezesha vijana katika nchi yetu tofauti na hapo Wizara ya Ofisi ya Rais ina mfuko wa vijana, Wizara nyingine inao. Hii inapunguza hata ufanisi wa mifuko yenyewe tofauti na endapo ingekuwa kwenye kapu moja ni rahisi kuiratibu"
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED