Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia kiasi cha Sh. bilioni 66.7 kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 619 vya mkoa huo, ambapo kaya 19,878 zinatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mtanda aliyasema hayo jana wakati wa kikao cha kuwatambulisha wakandarasi wa mradi huo ambao ni TIBEA Company Limited na White City International Contractors, waliokabidhiwa jukumu la kusambaza umeme katika vitongoji hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Amesisitiza kuwa mradi huo ni mkubwa na wa kimkakati, unaotarajiwa kunufaisha wananchi wa wilaya za Ukerewe, Misungwi, Magu, Sengerema na Kwimba. Hivyo, aliwataka wakandarasi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia sheria, huku akionya vikali dhidi ya vitendo vya rushwa wakati wa kuwaunganishia wananchi umeme.
“Ni muhimu mkafanya kazi kwa uadilifu na mkajiepushe na vitendo vya rushwa wakati wa kuwaunganishia wananchi umeme, kwani vitendo hivyo vinaharibu taswira ya kampuni zenu na vikibainika, sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kunyimwa kazi nyingine za Serikali,” alisema Mtanda.
Aidha, aliwaomba wananchi watakaonufaika na mradi huo kuwapokea vizuri wakandarasi na kushirikiana nao kwa karibu. Alisisitiza umuhimu wa wakandarasi kushirikisha ngazi zote za Serikali hadi kwa wananchi walengwa ili kurahisisha utekelezaji wa mradi, pamoja na kuwaelimisha wananchi kuhusu sifa za mradi na taratibu za kuunganishiwa umeme majumbani mwao ili kuepuka usumbufu na mianya ya rushwa.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Seif Abduli, alisema TIBEA Company Limited itahudumia vitongoji 313 katika wilaya za Sengerema na Kwimba kwa gharama ya Shilingi bilioni 33.7, huku White City International Contractors ikihudumia vitongoji 306 katika wilaya za Ukerewe, Misungwi na Magu kwa gharama ya Shilingi bilioni 32.7.
Mhandisi Seif aliongeza kuwa mradi huo ni wa kimkakati na unalenga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma ya umeme. Alisema Serikali imeleta kifaa maalum kiitwacho OMETA ambacho kitawasaidia wananchi wa vijijini wasiokuwa na uwezo wa kufanya wiring kuunganishiwa umeme, ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED