Leo Februari 3, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameanza ziara ya kikazi nchini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE), kwa kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na wadau wa kimataifa, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja nchini.
Katika ratiba ya leo, Rais Samia anakutana na Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, Gaston Browne, pamoja na kufanya mazungumzo ya pande mbili na Shaikha Al Nuwais, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism). Mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa hususan katika sekta ya utalii, biashara na uwekezaji.
Jioni ya leo, Rais Samia anatarajiwa kushiriki uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa maalumu la uwekezaji linalolenga kuoanisha miradi iliyo tayari kuwekezeka barani Afrika na wawekezaji wa kimataifa.
GAIS ni mpango wa kimkakati unaoendeshwa sambamba na majadiliano ya sera ya World Governments Summit (WGS), ukiwa na lengo la kubadili majadiliano ya sera kuwa uwekezaji halisi wenye matokeo chanya kwa maendeleo ya bara la Afrika.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED