ZAIDI ya watu 10,000 wenye ugonjwa wa kisukari wanahitaji dawa ya insulini ili kuendelea kuishi na kuboresha maisha yao, na watu hao ni kati ya Watanzania milioni 2.9 wanaoishi na kisukari nchini.
Hayo yameelezwa leo visiwani Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa kushughulikia changamoto na vikwazo vya upatikanaji na usambazaji wa dawa ya insulini ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Abdulla amesema kwa sasa Tanzania bara na Zanzibar zina zaidi ya kliniki 170 zenye jumla ya watoto 7,607 wanaoishi na kisukari aina ya kwanza kati yao 7,134 Tanzania bara na 473 Zanzibar.
Amesema dawa ya insulini ni dawa ya msingi ya kuokoa maisha ya watu wanaoishi na ugojwa wa kisukari duniani.
Hata hivyo, amesema licha ya ufanisi wake uliothibitika katika matibabu bado kuna changamoto kubwa ikiwemo kukosekana kwa usawa duniani katika upatikanaji wa insulini bora na zenye unafuu.
Aidha, amesema serikali inawajibu wa kuunda mazingira wezeshi kupitia sera madhubuti, ufadhili endelevu na ushirikiano unaohakikisha hakuba anayeachwa nyuma.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED