Nchemba aitaka suluhisho kilimo Afrika

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 03:51 PM Feb 03 2026
Nchemba aitaka suluhisho kilimo Afrika
Picha: Imani Nathaniel
Nchemba aitaka suluhisho kilimo Afrika

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo barani Afrika zinaendelea kuongezeka kwa kasi, hali inayohitaji suluhisho la pamoja na la haraka kutoka kwa nchi za Afrika na wadau wa maendeleo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kikanda wa Zana Endelevu za Kilimo, Dk. Nchemba amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kupunguza uzalishaji wa mazao, kuongeza hatari ya ukosefu wa usalama wa chakula, pamoja na kuibua changamoto ya matumizi ya ardhi kutokana na ongezeko la shughuli za kilimo na makazi ya watu.

Ameeleza kuwa bado kuna mtazamo potofu katika jamii unaoiona sekta ya kilimo kuwa ni ya wazee na wanawake pekee, huku vijana waliomaliza vyuo vikuu wakikosa motisha ya kujiunga na sekta hiyo kutokana na matumizi ya zana duni na za kizamani. Amesisitiza kuwa vijana wanahitaji teknolojia na zana za kisasa ili kuvutiwa na kilimo chenye tija na faida.

Dk. Nchemba ameongeza kuwa sekta ya kilimo pia inakabiliwa na uhaba wa nguvu kazi, unaochangiwa na tija ndogo inayosababishwa na ukosefu wa teknolojia ya kisasa. Aidha, alisema wanawake wameendelea kubeba mzigo mkubwa wa shughuli za kilimo, hususan kilimo cha jembe la mkono, bila msaada wa zana za kisasa.

Amebainisha kuwa majadiliano ya mkutano huo yanatarajiwa kutoa suluhisho la changamoto hizo na kusaidia kupunguza mzigo unaoukabili sekta ya kilimo. Pia alisema uwekezaji katika kilimo barani Afrika bado haujaendana na mahitaji halisi ya wakati huu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesema mkutano huo ni wa kwanza wa aina yake, ukiwa na lengo la kujadili kwa kina masuala ya kilimo na usalama wa chakula. Alisema mkakati ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wanatumia trekta na zana za kisasa ili kuongeza uzalishaji.

Naye Waziri Daniel Chongolo amesema mkutano huo unatoa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora zitakazochangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Mkutano huo umehusisha wadau wa maendeleo, asasi zinazojihusisha na kilimo pamoja na washirika wa kimkakati, kwa lengo la kuweka mkakati wa pamoja wa matumizi ya zana za kisasa za kilimo na kuongeza thamani katika sekta hiyo.