Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 376 vya mkoa huo utawezesha uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo kupitia uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo vidogo katika maeneo ya wananchi.
Dendego ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumtambulisha rasmi mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya China Railway No. 4 Engineering Group Ltd kutoka Jamhuri ya Watu wa China, iliyoshinda zabuni ya kusambaza umeme katika vitongoji hivyo. Ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kufikia kaya 13,259 mara utakapokamilika.
Amesema upatikanaji wa umeme si anasa bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, akiongeza kuwa Mkoa wa Singida umeendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo kutokana na kuanzishwa kwa viwanda vidogo hadi ngazi ya vitongoji.
“Upatikanaji wa umeme utaongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia viwanda vidogo vidogo. Wananchi wa Mkoa wa Singida wana mahitaji makubwa ya umeme, hivyo idadi ya awali ya wananchi 13,000 ni mwanzo tu, na tunatarajia mahitaji yataongezeka zaidi,” amesema Dendego.
Aidha, amemtaka mkandarasi kutoa kipaumbele cha ajira za muda mfupi kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yatakayopitiwa na mradi huo.
Dendego alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini, baada ya kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 45.6 kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 376 vya Mkoa wa Singida.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Thomas Mmbaga, amesema Serikali kupitia REA imemtambulisha rasmi mkandarasi ili kuanza utekelezaji wa mradi huo kwa mkataba wa miaka mitatu. Ameeleza kuwa wateja wa awali 13,259 wanatarajiwa kuunganishwa na huduma ya umeme katika wilaya za Ikungi, Mkalama, Itigi, Iramba, Singida na Manyoni.
Naye mwakilishi wa Kampuni ya China Railway No. 4 Engineering Group Ltd, Mhandisi Baraka Mhagama, amesema kampuni hiyo imejipanga kutekeleza mradi huo ndani ya kipindi cha miaka miwili licha ya mkataba kuruhusu utekelezaji kwa miaka mitatu. Ameahidi kushirikiana kwa karibu na REA, TANESCO pamoja na viongozi wa Mkoa wa Singida ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta tija iliyokusudiwa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED